NEMC, wanahabari kushirikiana kuelimsha jamii Mtwara
25 May 2024, 22:36 pm
Mabadiliko ya tabia yanasababishwa na vyanzo vya asili na shughuli za binadamu ambazo changamoto kubwa zinazoleta na mabadiliko hayo ni Pamoja na kuongezeka kwa kiwango cha joto duniani ,misimu ya mvua isiyotabirika na kuongeze kwa kina cha bahari.
Na Musa Mtepa
Waandishi wa Habari mkoani Mtwara wameombwa kuwa na ushirikiano na Baraza la usimamizi na uhifadhi wa Mazingira (NEMC ) kwa ajili ya kutoa Elimu juu ya utunzaji wa mazingira na namna ya kukabiliana na changamoto za athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Wito huo umetolewa leo tarehe 25/5/2024 na afisa kutoka ofisi ya baraza la usimamizi na uhifadhi wa mazingira (NEMC) kanda ya kusini Mhandisi Msafiri Laurent kwenye maadhimisho ya siku ya uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani yaliyofanyika katika ukumbi wa chama cha walimu Tanzania (CWT) ambapo amesema kuwa kwa wakati wowote wanapohitaji kufanyakazi na NEMC ofisi ipo wazi kwa ajili ya ushirikiano huo katika kuzungumza na kutoa Elimu kwa jamii juu ya namna ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.
Pia Mhandisi Msafiri amesema kuwa mabadiliko ya tabia nchi yamekuwa yakileta athari kubwa katika jamii yanayochangiwa na matumizi ya nishati isiyo safi ikiwemo athari za kimazingira,kiafya na ya kijamii.
Kwa upande wake afisa ufuatiliaji na tathmini kutoka kituo cha msaada wa kisheria kwa wanawake na Watoto (NERIO) mkoa wa Mtwara Bi Judith Chitanda amesema mabadiliko ya tabia nchi na ukatili wa kijinsia hasa kwa upande wa wanawake wamekuwa wahanga wakubwa katika kusababisha kuvunjika kwa ndoa pamojana na vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Naye Asia kilambwanda Mwandishi wa Habari kutoka redio Ahamadia Mtwara amesema waandishi na vyombo vya Habari vinajukumu katika kuelimisha na kuhamasisha jamii mgawanyo wa majukumu kijinsia katika kuhakikisha mambo yote yanayohusisha suala la mazingira wanaume wanashiriki ili kupunguza athari zinazojitokeza kwa upande wa wanawake.
Aidha katibu mtendaji wa chama cha waandishi wa Habari mkoa wa Mtwara (MTPC) Brayson Mshana ameelezea dhamira ya kufanya maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya Habari Duniani pamoja na wadau walioshiriki katika maadhimisho hayo.