RC Mtwara, wananchi wafanya usafi
25 May 2024, 15:22 pm
Wananchi wengi wameonesha kufurahishwa kwa kitendo cha viongozi wa serikali ya mkoa na wilaya ya Mtwara kuungana nao katika zoezi zima la usafi na wengi wao wakisema kuwa watakuwa na mwendelezo wa zoezi hilo majumbani mwao
Na Musa Mtepa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala leo tarehe 25/5/2024 ameongoza Wananchi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani katika zoezi la usafi lililofanyika katika Barabara ya Mnarani –Magomeni na eneo la makaburi msafa.
Aidha zoezi hilo lililotanguliwa na matembezi ya mwendo wa pole (Jogging) iliyoanzia katika ofisi za mkuu wa mkoa kuelekea Parishi,Bandarini ,Soko kuu hadi viwanja vya sabasaba ambapo akiwa katika viwanja hivyo amewapongeza Wananchi kwa kujitokeza kwa uwingi huku akiwa na matarajio ya kuwa zoezi hilo litakuwa endelevu kwa kila inapofika jumamosi ya mwisho ya kila Mwezi.
Pia Mkuu wa mkoa Kanali Patrick Sawala ametumia nafasi hiyo kuwaomba Wananchi kuendelea kutunza amani iliyopo na kuvipongeza vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuendelea kuifanya Mtwara na Tanazania kuwa salama.
Nao baadhi ya Wananchi waliojitokeza katika zoezi la usafi wameonesha kufurahishwa na kumpongeza mkuu wa mkoa kwa kitendo hicho cha kuwakutanisha na kufanya usafi Pamoja huku wengine wakisema kuwa zoezi hilo liwe endelevu kama linavyofanyika katika mikoa mingine.
Zoezi la usafi lililotanguliwa na matembezi ya mwendo wa pole yamehusisha wananchi,viongozi wa Serikali na vyama vya siasa Pamoja na vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Manispaa ya Mtwara Mikindani