TPA yaiomba serikali Bandari ya Mtwara kuunganishwa na Reli
25 March 2024, 17:26 pm
Changamoto zinazoikabili Bandari ya Mtwara ni kutokuunganishwa na miundombinu ya Reli pamoja na Barabara ya Mtwara –Dar es Salaam kutokuwa vizuri kuwezesha Bandari hiyo kuunganishwa na miundombinu hiyo.
Na Musa Mtepa
Naibu mkurugenzi mkuu wa mamlaka ya usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) Mhandisi Juma Kijavala amesema kuwa changamoto inayoikabili Bandari ya Mtwara ni ukosefu wa kuunganishwa na miundo ya Reli na Barabara hasa inayounganisha Mkoa wa Mtwara na Dar es saalam.
Hayo ameyasema leo 25/3/2024 kwenye ziara ya kamati ya Bunge ya kudumu ya uwekezaji wa mitaji ya umma ilipotembelea katika Bandari ya Mtwara kujionea uwekezaji ulifanywa na Serikali ambapo Mhandisi Juma Kijavala amesema changamoto zinazo wakabili zipo nje ya mamlaka ya Bandari ikiwa ni pamoja na kutokuunganishwa na miundombinu ya Reli pamoja na Barabara ya Mtwara –Dar es Salaam kutokuwa vizuri kuwezesha Bandari kuunganishwa na miundombinu hizo.
kwa upande wake mwenyekiti kamati ya Bunge ya kudumu ya uwekezaji wa mitaji ya umma Deus Clement Sangu amesema kuwa wataendelea kuishawishi serikali iweze kuboresha miundo mbinu ya Barabara na Reli ili miradi hiyo iweze kuwa na tija kwa Wananchi wa mikoa ya kusini na serikali kwa ujumla.
Akizungumzia faida ya uwekezaji uliofanywa na serikali katika Bandari hiyo Mkuu wa wilaya ya Mtwara Mwanahamisi Munkunda amesema kumekuwa na ajira wanazozipata vijana na akina mama wa ndani na nje ya Mtwara kutokana na uwekezaji huo.