Jamii FM

ADEA yaendelea na mafunzo ya sanaa ya uchoraji Mtwara

24 November 2024, 10:42 am

Hili ni kundi la pili katika utekelezaji wa programu ya Kuimarisha sanaa,utamaduni na ufundi stadi kwa vijana ambapo kundi la kwanza lilikuwa la uchongaji ambalo bado linaendelea na mafunzo kwa vitendo zaidi.

Na Musa Mtepa

Baadhi ya wasanii wa sanaa ya uchoraji wanaohudhuria mafunzo ya sanaa katika kituo cha makumbusho cha MAKUYA kilichopo chini ya shirika la ADEA mtaa wa Sinani, Manispaa ya Mtwara Mikindani, wameonesha kufurahi na kuwa na matumaini makubwa ya kupata manufaa baada ya kumaliza mafunzo hayo.

Wakizungumza Novemba 22, 2024, wamesema kuwa sanaa ya uchoraji ina changamoto kubwa, hasa kutokana na baadhi ya wachoraji kutokujua na kufuata utaratibu wa kimataifa wa sanaa hiyo.

Dastan Daniel, msanii wa sanaa ya uchoraji, amesema amepokea vyema mafunzo hayo kwani atajifunza mambo ambayo hapo awali alikuwa hayafahamu, na kuamini kuwa yatamsaidia kuboresha sanaa yake.

Sauti ya Dastan Daniel Msanii wa sanaa ya Uchoraji Manispaa ya Mtwara Mikindani

Amina Igugu, msanii mwingine wa uchoraji, amesema mafunzo hayo yatamuongezea ujuzi na kufungua fursa zaidi katika fani yake na kuwataka wasanii wengine kutumia nafasi kama hizi kujitokeza kwa wingi ili kujiongezea ujuzi na elimu mpya.

Sauti ya Amina Igugu Msanii wa sanaa ya uchoraji Manispaa ya Mtwara Mikindani

Mwezeshaji wa mafunzo hayo, Yasini Mukungu, amesema amewaandalia michoro na mbinu mbalimbali za kimataifa ambazo baadhi ya washiriki walikuwa hawajui.

Aidha, amewasisitiza wasanii hao kuzingatia vigezo vya kimataifa na kuhakikisha wanapata vifaa na mahitaji muhimu kwa ajili ya sanaa hiyo.

Sauti ya Yasini Mukungu mwezeshaji wa mafunzo ya uchoraji.

Mafunzo haya yanatolewa na shirika linalojihusisha na sanaa na utamaduni mkoani Mtwara, la ADEA, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa programu ya kuimarisha sanaa, utamaduni, na ufundi stadi kwa vijana. Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi, na Utamaduni (UNESCO) pamoja na Alwaleed Philanthropies ambayo yanatarajiwa kunufaisha takribani wasanii 50 kutoka katika fani mbalimbali za sanaa, ikiwemo uchoraji, uchongaji, ufundi seremala na ufundi chuma.