Jamii FM

TMA yasisitiza wakulima kutumia vizuri mvua zinazoelekea kanda ya kusini

24/03/2026, 11:48

Kaimu meneja TMA kanda ya kusini Elewa Msomba akiwa katika mahojiano kwenye kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na jamii fm radio Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wahimizwa kutumia vizuri mvua zinazoelekea kuisha kwa shughuli za maendeleo huku wakitakiwa kuchukua tahadhari na kuzingatia ushauri wa wataalamu wa hali ya hewa na kilimo ili kupata tija

Na Musa Mtepa

Wananchi wameshauriwa kutumia vizuri mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo yao kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo, zikiwemo kilimo, uvuvi na ufugaji, ili kuwawezesha kupata tija.

Hayo yamesemwa Machi 23, 2026 na Kaimu Meneja wa TMA Kanda ya Kusini, Bw. Elewa Msomba, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na Jamii FM Radio. Amesema kuwa kwa kuwa msimu wa mvua unaelekea mwishoni katika ukanda wa kusini, wananchi hawana budi kuzitumia ipasavyo ili kupata manufaa katika shughuli zao.

Sauti ya 1 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini

Aidha, Bw. Elewa Msomba amesema kuwa pamoja na msimu wa mvua kuelekea ukingoni katika ukanda wa kusini, hasa kwa wanaoishi maeneo ya bondeni na yenye unyevunyevu, wanapaswa kuchukua tahadhari kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika kipindi hiki cha mwezi wa tatu ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.

Sauti ya 2 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi kutoka Kituo cha Hali ya Hewa kilichopo katika Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI–Naliendele, Renatus Kapenda, amewataka wakulima kulima mazao kwa kuzingatia utabiri wa hali ya hewa unaotolewa na TMA pamoja na ushauri wa wataalamu wa kilimo waliopo katika maeneo yao, ili waweze kulima mazao yanayoendana na msimu husika.

Sauti ya 1 Renatus Kapenda Afisa TMA TARI–Naliendele

Sambamba na hilo, Renatus Kapenda amewataka wakulima kutambua kuwa mvua zinazoendelea kunyesha zinatarajiwa kuisha katika wiki ya nne ya mwezi Aprili na mwanzoni mwa mwezi Mei. Hivyo, ni muhimu kwa wakulima kuzingatia ushauri na kushirikiana na wataalamu wa kilimo ili kuelekezwa mbegu zinazofaa kulingana na kiasi cha mvua kilichobaki.

Sauti ya 2 Renatus Kapenda Afisa TMA TARI–Naliendele
Afisa mfawidhi kutoka kituo cha hali ya hewa katika kituo cha utafiti wa kilimo Tanzania TARI-Naliendele Renatus Kapenda akiwa katika studio za jamii fm radio (Picha na Musa Mtepa)

Kwa mujibu wa TMA, msimu wa mvua kwa mikoa ya kusini ulianza mwezi Disemba 2025 na unatarajiwa kumalizika katika wiki ya nne ya mwezi Aprili hadi wiki ya kwanza ya mwezi Mei, huku mvua hizo zikiwa chini ya wastani kulingana na rekodi za mvua katika mikoa hiyo.

Sauti ya 3 Elewa Msomba Kaimu Meneja TMA Kanda ya Kusini