Jamii FM
Jamii FM
24 January 2025, 22:50 pm

Na Musa Mtepa
Leo, Januari 24, 2025, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, amezindua rasmi kampeni ya msaada wa kisheria inayoendeshwa kwa jina la Samia Legal Aid Campaign katika viwanja vya Mashujaa Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akizungumza wakati wa uzinduzi, Kanali Sawala amesisitiza umuhimu wa wananchi kujitokeza kwa wingi kwenye viwanja hivyo pamoja na maeneo mengine yatakayotoa elimu kuhusu msaada wa kisheria.

Aidha Kanali Sawala amesema kuwa lengo kuu la kampeni hiyo ni kuwasaidia wananchi kufahamu haki zao za msingi na kuongeza uelewa wa masuala ya kisheria na haki za binadamu, hususani haki za wanawake, watoto, na watu wenye uhitaji.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Mtwara, Mhe. Rose Ibrahim, ametoa pongezi kwa kampeni hii na kusema kwamba Mahakama inajivunia kuwa ni mdau muhimu katika kampeni hii na kusisitiza kuwa wananchi wengi wanapohitaji huduma za kisheria au wanapohudhuria mahakamani, mara nyingi huwa hawajui nini cha kufanya, na hivyo kampeni hii ni fursa muhimu ya kujifunza na kupata uelewa kuhusu taratibu na haki zao za kisheria.
Pia, Jaji Rose Ibrahim amehimiza wananchi kutumia vizuri fursa ya kampeni hii ili waweze kujua zaidi kuhusu masuala ya kisheria na kujua hatua zinazofaa wanapokuwa na masuala ya kisheria.

Kampeni hii inaendelea kutoa elimu kuhusu msaada wa kisheria kwa wananchi na inatarajiwa kuwa na manufaa makubwa katika jamii ya Mtwara.
