Jamii FM
Jamii FM
23/03/2026, 14:20

Wananchi wamehimizwa kuzingatia taarifa za hali ya hewa kutoka TMA ili kuboresha shughuli zao. Elimu imetolewa kwa wanafunzi Naliendele, wakihamasishwa kuwa mabalozi wa taarifa hizo kwa familia na jamii.
Na Musa Mtepa
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) Kanda ya Kusini imeadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani katika Shule ya Sekondari Naliendele, huku ikiwataka wananchi kuwa na utamaduni wa kuzingatia taarifa zinazotolewa na mamlaka hiyo ili kufanikisha shughuli zao za kila siku.
Wito huo umetolewa leo Machi 23, 2026 na Tamimu Masai, afisa wa TMA Kanda ya Kusini, wakati wa maadhimisho hayo yaliyofanyika kikanda katika shule hiyo. Amesema lengo la maadhimisho ni kutoa elimu kwa wanafunzi kuhusu umuhimu wa hali ya hewa, ili waweze kufikisha ujumbe huo katika familia zao.
Tamimu amesema wananchi wanapaswa kufuatilia taarifa za hali ya hewa na kuzitumia ipasavyo, kwa kuwa zinamhusu kila mtu na kila shughuli ya maisha ya kila siku.

Aidha, amesema kuchagua Shule ya Sekondari Naliendele kumechangiwa na nia ya kuwahamasisha wanafunzi kupenda masomo ya sayansi, pamoja na kuwaandaa kuwa mabalozi wa kueneza ujumbe wa umuhimu wa kuzingatia taarifa za hali ya hewa zinazotolewa na TMA.

Baadhi ya wanafunzi wa shule hiyo wameeleza kufurahishwa na maadhimisho hayo, wakisema yamewasaidia kuongeza uelewa kuhusu hali ya hewa huku wakiwataka wazazi na wakulima kuzingatia taarifa zinazotolewa na wataalamu wa TMA kupitia vyombo vya habari.
