Jamii FM

Shekhe Mkuu Mtwara awataka wananchi kutunza amani kuelekea uchaguzi

23 February 2025, 11:11 am

Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ,Shekhe Jamaldin Chamwi akihutubia katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya msikiti mkuu Mkanaledi Manispaa ya Mtwara Mikindani(Picha na Musa Mtepa)

Mkutano wa hadhara wa shehe mkuu wa mkoa wa Mtwara ulikuwa hitimisho la ziara yake aliyoifanya katika kata ya Magomeni ,ambapo kabla ya mkutano huo alitembelea miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo Zahanati ya magomeni,Shule ya sekondari makanledi,Ujenzi wa Msikiti Muzdalifa yote iliyopo kata ya Magomeni Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Na Musa Mtepa

Shehe Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Shehe Jamaldin Chamwi, amewataka wananchi wa Mtwara na Tanzania kwa ujumla kutunza amani iliyopo na kujifunza kutokana na hali inayoendelea katika baadhi ya nchi baada ya matokeo ya uchaguzi.

Ametoa wito huo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika Februari 21, 2025, katika viwanja vya msikiti mkuu wa Mkanaledi ambapo Shehe Chamwi amesisitiza kuwa mtu mwenye akili na busara ni yule anayejifunza kutokana na kile kilichowapata wengine, akihusisha baadhi ya nchi ambazo zimeingia kwenye migogoro baada ya uchaguzi mkuu.

Sauti ya 1 Shehe Jamaldin Chamwi ,shehe mkuu wa mkoa wa Mtwara
Shehe Jamaldin Chamwi akikabidhi cheti cha uhitimu wa mafunzo ya kuosha na kutengeneza Sanda ya maiti kwa moja ya washiriki wa mafunzo hayo .

Aidha, Shehe Chamwi amewaasa wananchi kutii viongozi na mamlaka kama inavyotakiwa, akisema kuwa Uislamu unafundisha kutii viongozi, hata kama kiongozi huyo anakuwa na sifa duni.

Sauti ya 2 Shehe Jamaldin Chamwi ,shehe mkuu wa mkoa wa Mtwara.

Amesisitiza kuwa amani ni muhimu, na kuwataka Waislamu kuendelea kulinda mshikano wa dini, bila kujali itikadi za vyama vya kisiasa, kwani vyama havipaswi kuwa kikwazo cha kuwatenganisha waumini na Mwenyezi Mungu pamoja na Mtume Muhammad (S.A.W).

Pia, Shehe Chamwi amezungumzia suala la wanafunzi kutokuwa na muda wa kujifunza dini ya Kiislamu kutokana na ratiba za masomo shuleni,Akisema kuwa suala hilo limelifikishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwamba wakati wowote linaweza kupatiwa ufafanuzi.

Sauti ya 3 Shehe Jamaldin Chamwi ,shehe mkuu wa mkoa wa Mtwara.

Wakizungumzia nasaha za Shehe Chamwi, baadhi ya waumini waliohudhuria mkutano huo wamekubaliana na kauli ya kutunza amani huku wakisisitiza kuwa vurugu zikitokea, athari kubwa zitawaathiri wanawake na watoto.

Sauti ya baadhi ya waumini wakielezea suala la kutunza na kulinda amani kuelekea uchaguzi mkuu.

Katika mkutano huo, Shehe Chamwi pia amekabidhi vyeti kwa wanawake wa Kiislamu waliohitimu mafunzo ya kuosha maiti na kuandaa sanda ya marehemu na kuwataka kuyatilia maanani mafunzo hayo muhimu.