Jamii FM
Jamii FM
22 July 2025, 12:04 pm

Moto umeteketeza nyumba tano katika kijiji cha Mnaida, kata ya Tangazo, Mtwara Vijijini huku zingine mbili zikiezuliwa ili kuzuia kuenea kwa moto huku chanzo chake kikiwa bado hakijajulikana na uchunguzi unaendelea wakati huo Serikali na taasisi mbalimbali zimeanza kutoa msaada kwa waathirika
Na Musa Mtepa
Takribani nyumba tano zimeteketea kwa moto, huku nyingine mbili zikilazimika kubomolewa kwa hiari ili kuzuia moto kuenea zaidi, katika tukio lililotokea Julai 20, 2025 katika kijiji cha Mnaida, kata ya Tangazo, Halmashauri ya Mtwara Vijijini.Chanzo cha moto huo bado hakijafahamika rasmi, ingawa uchunguzi unaendelea kufanywa na vyombo husika.
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, moto ulianza majira ya mchana ukitokea kwenye banda la kupikia lililokuwa nyuma ya moja ya nyumba zilizoungua.
Bai Abdala Namwenyewe, mmoja wa waathirika, amesema alipokea taarifa za kuteketea kwa nyumba yake wakati akiwa kisiwani Bahasha, baada ya kupigiwa simu na kuambiwa nyumba yake inaungua.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa kijiji cha Mnaida, Juma Mega, amesema wananchi wameanza kujitokeza kutoa msaada wa chakula na malazi ya muda kwa waathirika, huku akiishukuru serikali kwa kuwafikia kwa haraka.
Kwa upande wake, Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Mtwara, Ambros Ndunguru, ametoa rai kwa wananchi wa kata ya Tangazo kuhakikisha wanatoa taarifa mapema pindi ajali za moto zinapotokea, na kuwataka kina mama kuwa waangalifu wakati wa shughuli za upishi kwa kuzima moto mara baada ya kumaliza.
Naye Ruge Sezi, Mratibu wa Shirika la Msalaba Mwekundu (Red Cross) mkoa wa Mtwara, amesema baada ya kupokea taarifa za kuungua kwa nyumba hizo tano, walifika kijijini kwa ajili ya tathmini na kutoa msaada wa makazi ya muda kwa waathirika.
Akiwapa pole wananchi waliopoteza makazi yao, Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdala Mwaipaya, amesema kamati ya maafa ya wilaya imefanikiwa kufikisha misaada ya haraka kwa waathirika, ikiwemo chakula, magodoro na vyandarua.
Ametoa wito kwa wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu huku hatua nyingine za msaada zikiendelea.

