Jamii FM
Jamii FM
22 February 2026, 18:19 pm

Vijana wahimizwa kutumia mitandao kwa maadili na kulinda amani wakati wa Maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani yaliyofanyika Mtwara , yakikumbuka miaka 160 ya Robert Stephenson Baden-Powell
Na Musa Mtepa
Vijana wametakiwa kutumia mitandao ya kijamii kwa kuzingatia maadili, tamaduni na mila za Kitanzania, na kuitumia kwa manufaa yao binafsi pamoja na taifa kwa ujumla. Pia wametakiwa kuachana na maudhui yanayoharibu maadili, utu, tunu za taifa, pamoja na yale yanayochochea uvunjifu wa amani.
Nasaha hizo zimetolewa leo Februari 22, 2026 na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara , ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani yaliyofanyika kitaifa katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara.
Bi. Telack amewataka vijana kutumia teknolojia kwa hekima na busara, pamoja na kupambanua maudhui yanayopatikana kwenye mitandao ya kijamii, na kuachana na yale yote yanayoharibu imani za dini, maadili na tamaduni za Kitanzania.

Aidha, Bi. Telack ameendelea kusisitiza umuhimu wa vijana kuipenda na kuilinda amani iliyopo nchini kwa kuwa na uzalendo wa kweli kwa Tanzania. Alisema hakuna nchi nyingine kwao zaidi ya Tanzania, hivyo ni wajibu wa kila kijana kuhakikisha anailinda na kuipambania nchi yake.

Akisoma risala mbele ya mgeni rasmi, Sarah Vanessa, mwakilishi wa Skauti Mkoa wa Mtwara, amesema pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kupitia Skauti bado kuna changamoto mbalimbali zinazowakabili zikiwemo ufinyu wa bajeti ya kusaidia vijana wa skauti kutekeleza miradi ya uzalishaji mali, pamoja na ukosefu wa vifaa vya uokoaji kwa timu za maafa katika wilaya na mikoa.

Akitoa salamu kwa niaba ya Bodi ya Skauti Tanzania, mwakilishi kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Ndugu Lazaro Mkeni, amesema wizara itaendelea kusimama pamoja na Chama cha Skauti Tanzania kuhakikisha misingi ya kuanzishwa kwa chama hicho inalindwa na kuimarishwa. Ameongeza kuwa wizara ipo tayari kutoa msaada pale inapobidi ili kuhakikisha misingi hiyo inasimamiwa ipasavyo.

Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Komredi Ibrahim Mjanaheri Ibrahim, amewapongeza waandaaji wa maadhimisho hayo,huku akitoa rai kwa vijana kuendelea kudumisha amani na kuachana na mtu yeyote anayetaka kuivuruga amani ya nchi.

Maadhimisho ya Siku ya Skauti Duniani Kitaifa kwa mwaka 2026 yamefanyika katika viwanja vya Nangwanda Sijaona mkoani Mtwara, yakiwa na kaulimbiu isemayo: “Elimu Bunifu na Stadi za Kidijitali kwa Maendeleo Endelevu ya Vijana.”
Maadhimisho hayo ni kumbukizi ya miaka 160 tangu kuzaliwa kwa mwanzilishi wa Skauti Duniani, Robert Stephenson Baden-Powell, mzaliwa wa Uingereza, aliyezaliwa Februari 22, 1857. Alianzisha Skauti mwaka 1907 na baadaye mwaka 1908 akaandika kitabu maarufu kiitwacho Scouting for Boys.
Baden-Powell alianza kwa kufanya kambi ya majaribio mwaka 1907 katika Kisiwa cha Brownsea, Uingereza, ambapo alitoa mafunzo kwa vijana yenye lengo la kuwafundisha uongozi, kujitegemea, uzalendo na huduma kwa jamii. Harakati hizo zilisambaa duniani kote, kama ambavyo leo zimeadhimishwa mkoani Mtwara na Tanzania kwa ujumla.
