Waandishi wa habari, wadau wafanya usafi Mtwara
21 September 2024, 16:15 pm
Hii ni Siku ya usafi Duniani ambapo chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara (MTPC) kwa kushirikiana na ofisi ya Mkurugenzi Manispaa ya Mtwara Mikindani, Ofisi ya Mbunge Mtwara Mjini ,Mganga mkuu wa mkoa na Wadau wengine wamefanya usafi katika soko la feri Manispaa ya Mtwara Mkindani ikiwa ni sehemu ya kuendeleza juhudi za kuunga mkono jamii katika shughuli mbalimbali za kimaendeleo
Na Musa Mtepa
Waandishi wa habari mkoani Mtwara wameungana na wadau mbalimbali kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani kwa kufanya usafi katika soko la Ferry, Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Wadau walioshiriki katika zoezi ni pamoja na Ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Taasisi ya Uhifadhi wa Bahari na Maeneo Tengefu, pamoja na wafanyabiashara wa samaki wa soko hilo.
Akizungumza kuhusu zoezi hilo, Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Bi. Shadida Ndile, amewataka wananchi kuzingatia usafi katika maeneo yao ili kujikinga na magonjwa yanayoweza kujitokeza kutokana na uchafu.
Aidha, Meya amewakumbusha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa, kuanzia katika zoezi la uhakiki na uhuishaji wa taarifa katika daftari la kudumu la wapiga kura.
Maguri Wambura kutoka ofisi ya NEMC Kanda ya Kusini amesisitiza umuhimu wa kutunza mazingira kwa kupunguza matumizi ya kuni na kutumia nishati safi ya kupikia.
Kwa upande wake, Afisa Afya wa Manispaa ya Mtwara, Bi. Angelina January, kwa niaba ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, amewakumbusha wananchi kuchukua tahadhari dhidi ya ugonjwa wa homa ya Nyani (Mpox), ambao umekuwa ukiripotiwa katika baadhi ya nchi barani Afrika.
Haroun Chizi, mfanyabiashara wa Samaki soko la samaki Ferry, ameelezea shukrani zake kwa kufanya usafi katika eneo hilo na kuhimiza jamii kuwa na utamaduni wa usafi hata kwenye makazi yao.
Naye Katibu wa Waandishi wa Habari Mkoa wa Mtwara, Bryson Mshana, amesema kuwa zoezi hilo ni sehemu ya juhudi za kuwahudumia wananchi na kuendeleza ushirikiano katika masuala ya mazingira, ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Usafi Duniani.