Jamii FM
Jamii FM
21 June 2025, 12:01 pm

Hii ilikuwa sehemu ya kipindi kilichofanyika redioni kuelekea maadhimisho ya wiki ya Mazingira Duniani ambapo NEMC iliwasihi wananchi kutumia vifungashio vinavyokubalika kisheria ili kulinda mazingira, huku ikiendelea kutoa elimu kuhusu madhara ya mifuko ya plastiki na umuhimu wa utunzaji wa mazingira
Na Musa Mtepa
Wananchi wametakiwa kuhakikisha wanatumia vifungashio vinavyostahili kwa ajili ya kulinda na kuhifadhi mazingira, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kitaifa za kupambana na uchafuzi wa mazingira unaosababishwa na matumizi mabaya ya mifuko ya plastiki.
Hayo yamesemwa na Bi. Nelusigwe Mwanjabeki, Afisa Ustawi wa Jamii Mwandamizi kutoka Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), kanda ya kusini, alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na 90. Jamii FM Redio.
Amesema NEMC inaendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi sahihi ya vifungashio kupitia kampeni mbalimbali katika masoko na vyombo vya habari, ili kuhakikisha kila mwananchi anakuwa na uelewa sahihi kuhusu utunzaji wa mazingira.
Bi. Nelusigwe ameongeza kuwa vifungashio vinavyofaa ni vile vilivyo na alama za ubora na maelezo ya bidhaa kama vile sukari, chumvi na vinginevyo vinavyoonyesha mzigo halisi unaobebwa pamoja na nembo ya utengenezaji.
Akijibu swali kutoka kwa msikilizaji aliyependa kufahamu mikakati ya kufikisha elimu ya mazingira hadi vijijini, Bi. Nelusigwe amesema kumekuwa na vitu mbalimbali vinavyofanywa ili kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa juu ya matumzi ya mifuko ya plastiki na athari zake.
Kwa upande wake, Bw. Muungano Senyagwa, Afisa Mazingira kutoka ofisi ya NEMC kanda ya kusini, amesisitiza kuwa katazo la matumizi ya mifuko ya plastiki lipo kwa mujibu wa sheria, kama ilivyoelezwa katika tangazo la serikali lililotolewa tarehe 1 Juni, 2019 kupitia Gazeti la Serikali.