Jamii FM
Jamii FM
21 February 2026, 18:34 pm

Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, amewataka wadau wa kilimo kushirikiana kuwawezesha wakulima kulima kisasa ili kuongeza tija. Wito huo umetolewa kwenye warsha ya Shoroba za Kilimo kwa mikoa ya kusini, ikisisitiza ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi
Na Musa Mtepa
Wadau wa kilimo wametakiwa kushirikiana kwa umoja katika kumsaidia mkulima kuzalisha kilimo chenye tija kwa kuwawezesha kulima kwa njia za kisasa, ikiwemo kuwapatia vitendea kazi bora vya kilimo.
Hayo yamesemwa Februari 20, 2026 na Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Zainab Telack, wakati akifungua Warsha ya Wadau wa Kilimo ya kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uendelezaji na ukuzaji wa Shoroba za Kilimo kwa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara, iliyofanyika mjini Mtwara.
Bi. Telack amesema kuwa mafanikio yaliyopatikana katika zao la korosho, ambapo wakulima wamezalisha zaidi ya shilingi bilioni 260, yanaonesha kuwa inawezekana pia kuongeza uzalishaji wa mazao mengine endapo wakulima watawezeshwa kulima kisasa. Amesisitiza matumizi ya matrekta na zana bora za kilimo ili kuwawezesha wakulima kulima mashamba makubwa zaidi na kuongeza tija.

Aidha, amewataka wakuu wa wilaya, wakuu wa idara za kilimo na sekta binafsi kutumia warsha hiyo kama fursa ya kujifunza, kubadilishana uzoefu na kuweka mikakati imara ya utekelezaji wa mageuzi ya sekta ya kilimo kwa mikoa ya kusini na taifa kwa ujumla.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Kuendeleza Kilimo kwa utaratibu wa Shoroba Tanzania (AGCOT), Geoffrey Kirenga, amesema lengo la warsha hiyo ni kuimarisha ushirikiano kati ya sekta binafsi na sekta ya umma pamoja na kuongeza ukaribu baina yao ili kukuza sekta ya kilimo.

Kirenga ameongeza kuwa katika warsha hiyo ameguswa na hoja zilizotolewa na sekta binafsi pamoja na viongozi wa halmashauri kwamba mwaka 2026 huenda malengo ya uzalishaji yasifikiwe kama ilivyotarajiwa kutokana na uhaba wa mbegu bora za ufuta. Amesema hali hiyo inaashiria kuongezeka kwa idadi ya wakulima wa zao hilo ikilinganishwa na miaka ya nyuma.
Kwa upande wao, Mkuu wa Idara ya Kilimo Halmashauri ya Masasi, James Chitumbi, pamoja na Mkuu wa Idara ya Kilimo Halmashauri ya Nachingwea, Rafael Magetu, wamesema warsha hiyo imewapa manufaa makubwa, ikiwemo namna ya kukabiliana na changamoto ya uhaba wa mbegu bora za mazao ya chakula na biashara kwa kuongeza juhudi za uzalishaji ili kufikia kilimo chenye tija.

Akifunga warsha hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brig Jenerali ,Ahmed Abbas, ametoa wito kwa wakuu wa wilaya kwenda kujifunza mbinu za kilimo-biashara zinazotekelezwa mkoani Lindi ili kukuza kilimo mseto na biashara katika Mkoa wa Ruvuma.

Warsha hiyo ya siku moja imewakutanisha wakuu wa mikoa, wakuu wa wilaya, wakuu wa idara za kilimo, sekta binafsi pamoja na wadau wa kilimo kutoka mikoa ya Lindi, Ruvuma na Mtwara. Lengo kuu lilikuwa kujenga uelewa wa pamoja kuhusu uendelezaji na ukuzaji wa Shoroba za Kilimo katika mikoa hiyo.
