Jamii FM

Wazazi wahimizwa kulea watoto kimaadili kuzuia mimba kwa wanafunzi

21 January 2026, 12:29 pm

Baadhi ya wazazi wa kijiji cha Nanguruwe wakishiriki kipindi cha wazi juu ya ni kifanyike ili kutekeleza mimba kwa wanafunzi (Picha na Henry Abdala)

Wazazi wa kijiji cha Nanguruwe wameaswa kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kukabiliana na mimba kwa wanafunzi. Wito huo umetolewa na viongozi wa elimu, polisi na walimu kupitia kipindi cha Wazi cha Jamii FM Redio.

Na Musa Mtepa

Wazazi wameshauriwa kuwalea watoto wao katika maadili mema ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanafunzi, ikiwemo mimba za utotoni zinazosababisha baadhi yao kusitisha masomo wakiwa shuleni.

Ushauri huo umetolewa na Afisa Elimu Kata ya Nanguruwe, Omari Makiluli, aliposhiriki kipindi cha Wazi kinachorushwa na Jamii FM Redio tarehe Januari 17, 2026. Kipindi hicho kilifanyika katika eneo la stendi ya magari kijijini Nanguruwe, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara.

Akichangia mada iliyokuwa ikijadiliwa ya “Nini kifanyike ili kutekeleza sera na mikakati ya serikali juu ya kutokomeza mimba kwa wanafunzi”, Makiluli amesema kumekuwepo na ombwe kubwa la wazazi na walezi katika kuwafuatilia mienendo ya watoto wao. Ameeleza kuwa ni muhimu wazazi kuwa karibu na watoto wao na kuwakuza katika maadili mema ili kuwaepusha na vishawishi vinavyoweza kuathiri maisha yao ya kielimu.

Sauti ya 1: Omari Makiluli, Afisa Elimu Kata ya Nanguruwe

Aidha, Afisa Elimu huyo amewasisitiza wazazi kuwahimiza watoto wao, hususan wa kike, kuendelea na masomo kwa kuhakikisha wanakwenda shule na kupata elimu itakayowawezesha kukabiliana na changamoto mbalimbali za kimaisha zinazojitokeza katika jamii.

Sauti ya 2: Omari Makiluli, Afisa Elimu Kata ya Nanguruwe

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nanguruwe, Mwalimu Keneth Kawinda, amesema kuwa ili kukabiliana na tatizo la mimba kwa wanafunzi, wazazi wanapaswa kuamini kuwa hosteli ni maeneo salama kwa watoto wao. Aidha amewataka wazazi kutoacha watoto wao uhuru wa kujiamulia kufanya mambo yasiyofaa bila usimamizi.

Sauti ya Mwalimu Keneth Kawinda, Kaimu Mkuu wa Shule ya Sekondari Nanguruwe

Naye Afisa wa Jeshi la Polisi Kata ya Nanguruwe, WPO Titus Julius Godfrey, amesema utekelezaji wa sera na mikakati ya serikali juu ya kuondoa mimba kwa wanafunzi unahitaji ushirikiano wa karibu kati ya wazazi, walimu na wanafunzi wenyewe ili kuzungumza lugha moja na kumsaidia mtoto kufikia malengo yake ya kielimu.

Sauti ya WPO Titus Julius Godfrey, Afisa wa Jeshi la Polisi Kata ya Nanguruwe

Kwa upande wao, baadhi ya wazazi na wananchi waliohudhuria kipindi hicho wamekiri kutokuwa karibu vya kutosha na watoto wao, huku wengine wakiahidi kuanza upya kwa kuzungumza na watoto wao kuhusu umuhimu wa elimu na njia za kujiepusha na mimba wakiwa shuleni.

Sauti ya wazazi na wananchi wa Kijiji cha Nanguruwe

Kipindi cha Wazi kinachoratibiwa na Jamii FM Redio kilianza rasmi Oktoba 9, 2025 katika Kata ya Naliendele, Manispaa ya Mtwara Mikindani, kikiwa na mada isemayo “Nini kifanyike ili jamii ishiriki kikamilifu kupunguza tatizo la mimba kwa wanafunzi shuleni”, Januari 17, 2026 kimefanyika katika Kijiji cha Nanguruwe, Halmashauri ya wilaya ya Mtwara kilichokuwa na mada isemayo “Nini kifanyike ili kutekeleza sera na mikakati ya serikali kuzuia mimba kwa wanafunzi shuleni”, huku kipindi kijacho kinachotarajiwa kufanyika Januari 24, 2026 katika Kijiji cha Majengo, Kata ya Ziwani, kikijadili mada ya “Nini kifanyike ili shughuli za kiuchumi zisiwe chanzo cha wanafunzi kupata mimba na kuacha shule”.

Lengo kuu la vipindi hivi ni kutoa elimu kwa jamii, kuhimiza uwajibikaji kwa kila mmoja na kumwezesha mwanafunzi, hususan mtoto wa kike, kutimiza malengo yake kupitia elimu.