Jamii yatakiwa kuelewa umuhimu wa malezi ya watoto
20 June 2024, 18:56 pm
Uelewa wa jamii juu ya masuala ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto kwa wenye umri wa miaka 0-8 ni jambo muhimu katika kuirejesha jamii katika mstari wa malezi sahihi ya watoto.
Na Mwanahamisi Chikambu
Uelewa juu ya masuala ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto wenye umri wa miaka 0-8 ni jambo muhimu katika kuirejesha jamii katika mstari wa malezi sahihi ya watoto nchini.
Hayo yameelezwa na Edwad Biashara ambaye ni mkufunzi wa program ya malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto katika mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari katika masuala ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) mkoani Mtwara yaliyofanyika jana 19.6.2024 katika ukumbi wa TCCIA mkoani hapa.
Kwa upande wake afisa ustawi wa jamii kutoka ofisi ya mkuu wa mkoa wa Mtwara ambae pia ni mratibu wa program ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (PJT-MMMAM) Teresia Ngonyani ameiomba jamii kuwekeza kwa watoto kuanzia umri wa miaka 0-8 ili kuhakikisha watoto hao wanakuwa katika ukuaji timilifu na kuwapa matunzo na malezi bora.
Wakizungumza mara baada ya mafunzo hayo baadhi ya waandishi wa habari kutoka mkoani mtwara waliohudhuria katika mafunzo hayo wamesema kwamba kutokana na elimu waliyoipata watakwenda kuelimisha jamii juu malezi makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto.
Programu Jumuishi ya Kitaifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ilizinduliwa Dodoma na aliyekuwa waziri wa Afya kipindi kile Dk Dorothy Gwajima kwa niaba ya Rais Samia Suluhu Hasaan mwaka 2021.