

20 March 2025, 09:13 am
Mradi wa Amani Yetu Kesho Yetu unaonekana kuwa ni hatua nzuri ya kujenga jamii yenye umoja na amani, hasa kwa kuhusisha vijana na wanafunzi ambao wapo katika hatari ya kutumbukia katika uvunjifu wa amani katika jamii
Na Musa Mtepa
Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Safety Alliance (TASA) limezindua rasmi mradi wake mpya wa “Amani Yetu Kesho Yetu” katika kata tano za Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara.
Mradi huu unalenga kuhamasisha amani na utulivu katika maeneo hayo kwa kushirikisha vijana na wanafunzi.
Mratibu wa mradi huo, Betty Chenge, amezungumzia umuhimu wa mradi huu kwa kusema kwamba utatekelezwa kwa mpango wa pande mbili, ambapo upande mmoja utahusisha wanafunzi, na mwingine utahusisha vijana waliopo mitaani.
Aidha Betty Chenge amesema mradi umehusisha vijana na Wanafunzi kutokana na makundi hayo kuwa katika hatari kuingia katika uvunjifu wa amani katika Jamii
Kwa upande mwingine, viongozi wa vijiji kutoka kata zitakazohusishwa na mradi huo wamesema kuwa mafunzo yatakayotolewa kupitia mradi huu yana umuhimu mkubwa, hasa ikizingatiwa kuwa maeneo haya yapo mpakani , jambo ambalo linaweza kuwa na changamoto katika kudumisha amani.
Viongozi hao pia wameongeza kuwa mradi huu utakuwa na manufaa makubwa kwa jamii, hasa kwa vijana, kwani utawawezesha kuepuka kujiingiza katika vitendo vya vurugu na uvunjifu wa amani.
Mradi wa “Amani Yetu Kesho Yetu” una lengo la kutoa elimu ya amani na usalama, kuhamasisha uelewa kuhusu athari za uvunjifu wa amani, na kuhimiza ushirikiano kati ya vijana, wanafunzi, na jamii kwa ujumla.