Jamii FM

Mtwara kuadhimisha kitaifa siku ya Skauti Duniani

20 February 2026, 16:44 pm

Kaimu mkuu wa mkoa wa Mtwara ambae pia mkuu wa mkoa wa Lindi Bi Zainab Telack akizungumza na vyombo vya habari leo ofisini kwake mjiniMtwara(Picha na Musa Mtepa)

Mkoa wa Mtwara utaadhimisha Siku ya Skauti Duniani Februari 22, 2026, kumuenzi Robert Baden-Powell. Maadhimisho hayo yatajumuisha mafunzo, huduma za jamii na kampeni za uzalendo, huku vijana 400 wakitarajiwa kunufaika na elimu mbalimbali. Wananchi wamealikwa kushiriki katika viwanja vya Nangwanda Sijaona

NA Musa Mtepa

Mkoa wa Mtwara unatarajia kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Kitaifa ya Siku ya Skauti Duniani yatakayofanyika Februari 22, 2026, ikiwa ni sehemu ya kumuenzi mwanzilishi wa harakati za Skauti Duniani, Robert Baden-Powell.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Bi. Zainab Telack, amesema kuwa maadhimisho hayo ni sehemu ya historia ya zaidi ya miaka 100 ya Skauti, yenye lengo la kuwajenga vijana katika misingi ya uzalendo, uwajibikaji na kuipenda nchi yao.

Bi. Telack ameeleza kuwa katika kuelekea kilele cha maadhimisho hayo, tayari shughuli mbalimbali zimeanza kufanyika kupitia vijana wa Skauti, ikiwemo kambi za mafunzo ya ukakamavu, utoaji wa huduma za jamii pamoja na shughuli za utunzaji wa mazingira. Aidha, Februari 21, 2026, vijana hao wanatarajiwa kushiriki mafunzo yanayohusu uwajibikaji, uzalendo na masuala ya usalama.

Sauti ya 1 Bi Zainab Telack kaimu mkuu wa mkoa wa Mtwara

Katika hatua nyingine, Bi. Telack ametumia fursa hiyo kuwaalika wananchi wote wa Mtwara kushiriki kwa pamoja katika maadhimisho hayo yatakayofanyika katika Viwanja vya Nangwanda Sijaona, mjini Mtwara.

Sauti ya 2 Bi Zainab Telack kaimu mkuu wa mkoa wa Mtwara

Kwa upande wake, Naibu Kamishina wa Skauti Mkoa wa Mtwara, Sofia Malandi, amesema kuwa kufanyika kwa maadhimisho hayo kumeleta fursa mbalimbali kwa vijana na kwa mkoa kwa ujumla. Amefafanua kuwa elimu tofauti zinaendelea kutolewa, ikiwemo elimu ya kupinga rushwa na kuimarisha uzalendo, ambapo jumla ya vijana 400 wanatarajiwa kunufaika na mafunzo hayo.

Sauti ya Sofia Mlandi naibu kamishina wa Skauti mkoa wa Mtwara
kamishina wa Skauti mkoa wa Mtwara Sofia Mlandi akizungumzia shughuli zinazofanyika kuelekea maadhimisho hayo(Picha na Musa Mtepa)

Naye Afisa Utamaduni wa Mkoa wa Mtwara ambaye pia ni Mratibu wa maadhimisho hayo, Bi. Fatuma Mtanda, amesema kuwa maadhimisho hayo yanatarajiwa kuhudhuriwa na wageni kutoka mikoa mbalimbali ikiwemo Lindi, Ruvuma, Mbeya, Mjini Magharibi na Pwani. Ameongeza kuwa mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Bi. Zainab Telack.

Sauti ya Fatuma Mtanda mratibu wa maadhimisho
Mratibu wa maadhimisho ya siku ya Skauti Duniani , Bi. Fatuma Mtanda akitolea ufafanuzi juu ya wageni watarajiwa na mgeni rasmi katika maadhimisho hayo(Picha na Musa Mtepa)