Jamii FM
Jamii FM
19 January 2026, 12:08 pm

Wananchi wa kijiji cha Nanguruwe wameiomba Serikali na wadau wa maendeleo kusaidia ujenzi wa soko la kisasa la bidhaa na vyakula ili kuboresha huduma za kibiashara. Ujenzi huo unafanywa kwa nguvu za wananchi na unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 70, huku wafanyabiashara zaidi ya 100 wakinufaika
Na Musa Mtepa
Wananchi wa kijiji cha Nanguruwe wameiomba Serikali pamoja na wadau wa maendeleo kuchangia na kusaidia ujenzi wa soko la bidhaa na vyakula unaoendelea kujengwa katika kijiji hicho.
Wakizungumza na Jamii FM Redio Januari 17, 2026, wananchi hao wamesema kuwa kutokana na ukuaji wa kasi wa kijiji chao, viongozi wa kijiji wameamua kuanzisha ujenzi wa soko la kisasa ili kuwaondolea adha wakazi wa kijiji hicho kutembea umbali mrefu kufuata huduma za kibiashara eneo la Barabarani.

Akizungumza kuhusu ujenzi wa soko hilo, Mwenyekiti wa Kijiji cha Nanguruwe, Bw. Saidi Mandova, amesema kuwa sababu kubwa ya uamuzi huo ni matumizi ya soko moja kwa vijiji vitatu kwa muda mrefu, hali iliyokuwa ikikisababishia kijiji kukosa mapato yatokanayo na shughuli za kibiashara.
Bw. Mandova ameongeza kuwa ujenzi wa soko hilo unatekelezwa kwa nguvu za wananchi wenyewe, huku akiomba wadau wa maendeleo kujitokeza kusaidia ili kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa.
Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji wa Kijiji cha Nanguruwe, Bw. Saidi Hamisi, ameelezea hatua za awali za utekelezaji wa mradi huo na kufafanua kuwa ujenzi unaendelea vizuri licha ya changamoto chache za upungufu wa rasilimali.
Ameongeza kuwa hadi kukamilika, ujenzi wa soko hilo unatarajiwa kugharimu shilingi milioni 70, huku zaidi ya wafanyabiashara 100 wakitarajiwa kunufaika na huduma za soko hilo.
