Jamii FM

Wakulima Mtwara waomba Serikali iwajengee daraja

18 July 2025, 10:47 am

Mwonekano wa Daraja Mtandoni lililojengwa na wananchi wakulima wa mazao ya kiangazi katika eneo Mwambo(Mbuyuni) katika kijiji cha Kilambo Mtwara Vijijini(Picha na Musa Mtepa)

Wakulima wa Mwambo (Mbuyuni), Kilambo – Mtwara Vijijini, wameiomba serikali kujenga daraja la kudumu Mtondoni kurahisisha kilimo, uvuvi na usafiri. Wanasema daraja la muda halitoshelezi, hasa masika, na linahatarisha usalama wa wakazi

Na Musa Mtepa

Wakulima katika eneo la Mwambo (Mbuyuni), Kijiji cha Kilambo, Halmashauri ya Mtwara Vijijini, wameiomba serikali na wadau wa maendeleo kujenga daraja la kudumu katika eneo la Mtondoni ili kurahisisha shughuli za kilimo, uvuvi na usafiri wa kila siku.

Wakizungumza na Jamii FM, wakulima hao wamesema kuwa eneo hilo ni muhimu kwa uzalishaji wa mazao mbalimbali na pia hutumiwa na wavuvi, lakini changamoto kubwa inayowakabili ni kuvuka mto hasa wakati wa masika, jambo linalohatarisha usalama wa wakazi.

Sauti ya Wakulima wa Mwambo(Mbuyuni) kilambo

Abdala Salumu Nalamba, mkazi wa Manispaa ya Mtwara Mikindani na mkulima katika eneo hilo, amesema kuna umuhimu mkubwa wa kujengwa kwa daraja la kudumu kwani wakulima na wafanyabiashara hulitumia daraja hilo mara kwa mara.

Aidha, Bw. Nalamba ameongeza kuwa kutokuwepo kwa daraja la uhakika kunasababisha wakulima kutumia kilimo cha mikono kwa sababu trekta hushindwa kufika mashambani kutokana na hali mbaya ya miundombinu.

Sauti ya Abdala Nalamba, mkulima wa eneo la Mwambo – Kilambo

Kwa upande wake, Mwenyekiti mstaafu wa Kitongoji cha Misifuni, Bw. Mfaume Amri, amesema kuwa wananchi wamejitolea kwa hali na mali kujenga daraja la muda, lakini sasa wanahitaji msaada rasmi kutoka serikalini au kwa wadau ili kuimarisha usalama wa watumiaji na kuendeleza shughuli za kiuchumi.

Sauti ya Mfaume Amri Mwenyekiti mstaafu wa kitongoji Misufini (Kilambo)