Jamii FM
Jamii FM
18/03/2026, 13:12

TAKUKURU Mtwara yaandaa Iftar kuimarisha uhusiano na jamii, viongozi wakisisitiza umoja, mshikamano na ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa wakati wa mwezi wa Ramadhani
Na Musa Mtepa
Ikiwa katika juhudi za kuimarisha uhusiano na utendaji wake pamoja na jamii inayoizunguka, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mtwara imejumuika na makundi mbalimbali katika kuandaa Iftar, huku ujumbe wa umoja na mshikamano ukitawala katika hafla hiyo.
Hafla hiyo iliyowakutanisha viongozi na wananchi wa kada mbalimbali imefanyika Machi 17, 2026, katika ukumbi wa mikutano wa Benjamin Mkapa uliopo katika Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (tawi la Mtwara), zamani Chuo cha Ualimu (TTC).
Akizungumza katika Iftar hiyo, mgeni rasmi ambaye ni Katibu Tawala wa Wilaya ya Mtwara, Wakili Richard Mwalingo, amewakumbusha wananchi umuhimu wa kuchukia vitendo vya rushwa na kuwa mstari wa mbele kutoa taarifa pindi wanapoona viashiria vya vitendo hivyo na kusisitiza kuwa ushiriki wa jamii ni silaha muhimu katika vita dhidi ya rushwa.

Naye Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Mtwara, Mashauri Elisante, amewashukuru wote waliojitokeza, akisema kuwa hafla hiyo inalenga kuimarisha uhusiano kati ya TAKUKURU na jamii, kwani taasisi hiyo imekuwa ikishirikiana na jamii katika utekelezaji wa majukumu yake.

Kwa upande wake, Katibu wa Jumuiya ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Mtwara, ambaye pia ni Askofu na Mchungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kusini Mashariki, Yeriko Nguema, amesisitiza umuhimu wa kuendelea kuimarisha umoja, amani na mshikamano miongoni mwa Watanzania bila kujali rangi, kabila au imani ya mtu.

Naye Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Sheikh Jamaldin Chamwi, amesema huruma, upendo na mshikamano ndivyo vinavyoimarisha misingi mikuu ya mwezi wa Ramadhani na kuongeza kuwa miongoni mwa mambo yanayokamilisha saumu ni pamoja na kufuturisha, kama ambavyo TAKUKURU imefanya.
