Jamii FM
Jamii FM
18/03/2026, 08:49

Waandishi wa habari 25 mkoani Mtwara wamepata mafunzo ya uhakiki wa taarifa kutoka Jamii Africa, yakilenga kuwasaidia kutambua taarifa sahihi na potofu ili kuboresha utoaji wa habari kwa wananchi
Na Musa Mtepa
Jumla ya waandishi wa habari 25 kutoka vyombo mbalimbali mkoani Mtwara wamepatiwa mafunzo ya uhakiki na uthibitishaji wa taarifa, yaliyotolewa na Jamii Africa chini ya taasisi mama ya Jamii Forums, kwa lengo la kuwawezesha kutambua taarifa potofu na zisizo sahihi katika jamii.
Wakizungumza baada ya mafunzo hayo yaliyofanyika Machi 17, 2026 mjini Mtwara, waandishi hao wameishukuru Jamii Africa kwa kuwapatia mafunzo hayo, wakisema yatawasaidia katika kazi zao za kila siku za kuhabarisha wananchi.
Aidha, waandishi hao wamesema kutokana na kukua kwa teknolojia, kumekuwa na changamoto ya watu kuzalisha maudhui ambayo kwa namna moja au nyingine husababisha mkanganyiko wa kutambua taarifa sahihi na zisizo sahihi hivyo, kupitia mafunzo hayo, wataweza kubaini ipi ni taarifa sahihi na ipi si sahihi.
Naye Afisa Programu kutoka Jamii Africa, Edward Chaina, amesema mafunzo ya uhakiki na uthibitishaji wa taarifa ni muhimu kwa waandishi wa habari kwa kuwa yatawawezesha kuwa na uelewa wa kutambua na kuthibitisha taarifa hizo, ili kuwasaidia wananchi kupata taarifa sahihi zitakazowawezesha kufanya maamuzi sahihi.
