Jamii FM

ATCL yarejesha safari za ndege Dar es Salaam, Mtwara

18 February 2025, 09:26 am

Mkuu wa wilaya ya Mtwara AbdaLA Mwaipaya akipanda Ndege ya Air Tanzania wakati wa uzinduzi wa urejesha huduma za usafiri wa Ndege za ATCL mkoa wa Mtwara(Picha na Musa Mtepa)

Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara Jordan Mchami amesema kutokana na kuwepo kwa gharama ndogo za nauli kwenda na kurudi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam ambayo ni shilingi 199,000, kutapelekea kuongezeka kwa abiria watakaotumia usafiri huo.

Na Musa Mtepa

Shirika la Ndege la Tanzania (ATCL) limerejesha huduma za usafiri wa ndege mkoani Mtwara, ambapo sasa ndege za shirika hilo zitakuwa zikifanya safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Mtwara mara tatu kwa wiki.

Uzinduzi wa safari hizi umefanyika tarehe 17 Februari, 2025, ambapo kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa ATCL, Arif Jihann, amesema kuwa hatua hii ni muhimu kwa maendeleo ya sekta ya usafiri wa anga nchini na inaleta fursa mpya kwa wakazi wa Mtwara na mikoa ya jirani.

Arif ameeleza kwamba uzinduzi wa safari hizi za moja kwa moja ni sehemu ya jitihada za kuboresha usafiri wa anga, na itasaidia kuongeza usafiri wa abiria kwa bei nafuu na kuboresha ufanisi wa huduma za usafiri wa ndege.

Sauti ya Arif Jihann kaimu mtendaji ATCL

Kwa upande mwingine, Meneja wa Uwanja wa Ndege wa Mtwara, Jordan Mchami, amesema kuwa hapo awali idadi ya abiria ilikuwa ndogo kutokana na gharama kubwa za usafiri, lakini ujio wa ATCL, na gharama za safari za kwenda Dar es Salaam na kurudi Mtwara zitakuwa Tsh 199,000, hivyo kuongeza idadi ya abiria watakaotumia ndege kutokana na gharama kuwa himilivu.

Sauti ya Jordan Mchami meneja wa uwanja wa ndege Mtwara

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdala Mwaipaya, aliyezindua safari hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, amesema kuwa wakazi wa Mtwara wamekuwa wakikumbwa na changamoto za usafiri baada ya kusitishwa kwa safari za moja kwa moja za Air Tanzania. Hata hivyo, kurejeshwa kwa safari hizi kunatambua dhamira ya serikali ya kufanya Mtwara kuwa lango kuu la uchumi wa Kusini.

Sauti ya Abdala Mwaipaya mkuu wa wilaya ya Mtwara

Baadhi ya abiria wamefurahi kurejea kwa safari za ndege za ATCL, wakisema kuwa gharama za usafiri zimepungua na sasa ni rahisi kwao kusafiri kwa ndege, hali ambayo inawavutia wengi kutumia njia ya anga kwa safari zao.

Sauti ya baadhi ya abiria waliosafiri kwa Ndege ya Air Tanzania