Jamii FM

Paka wa ajabu aibua taharuki Mtwara vijijini

17 February 2026, 20:09 pm

Paka wa ajabu aliyekutwa amekufa baada ya kudhaniwa kujipiga kwenye nyumba ya Bi Maimuna Abilahi mkazai wa kijiji cha Nangumi(Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa kitongoji cha Shangani, Nangumi, wamekumbwa na taharuki baada ya paka kupatikana amekufa na kuvalishwa hirizi katika nyumba ya mkazi mmoja. Tukio hilo limeibua hofu na maswali, huku viongozi wa kijiji wakieleza kusikitishwa na hali hiyo isiyo ya kawaida

Na Musa Mtepa

Wananchi wa kitongoji cha Shangani, kijiji cha Nangumi, kata ya Mayanga wilayani Mtwara Vijijini, wamekumbwa na taharuki baada ya kuonekana kwa paka aliyekufa huku mwilini mwake akiwa amevalishwa hirizi.

Tukio hilo limetokea alfajiri ya leo, Februari 17, 2026, katika nyumba ya Maimuna Abilahi, mchuuzi wa samaki na mkazi wa kijiji hicho.

Wakizungumza na Jamii FM Radio, baadhi ya wananchi wa Nangumi wameeleza kushangazwa na tukio hilo, huku wakilihusisha na imani za kishirikina. Wamedai kuwa paka huyo alionekana akiwa amejitupa katika eneo la nyumba hiyo, na baada ya kuchunguzwa alikutwa na hirizi shingoni na kiunoni.

Sauti ya wananchi wa Nangumi

Akizungumzia tukio hilo, Maimuna Abilahi, mmiliki wa nyumba hiyo, amesema alipata taarifa za tukio hilo kupitia simu alipokuwa feri kununua samaki kwa ajili ya biashara yake. Ameeleza kuwa aliondoka nyumbani mapema asubuhi akitumia mlango wa nyuma, ambao ni tofauti na eneo alikokutwa paka huyo.

Sauti ya Maimuna Abilahi, mmiliki wa nyumba

Kwa upande wake, baba mzazi wa Maimuna, mzee Abilahi Issa Mohamedi, amesema baada ya kupata taarifa hizo alifika eneo la tukio na kisha kumpigia simu mwanawe kumjulisha. Ameeleza kuwa walikubaliana kumchoma moto paka huyo majira ya saa kumi jioni.

Alipoulizwa sababu ya kusubiri hadi saa kumi jioni, mzee Abilahi amesema ni maagizo ya wataalamu, akidai kuwa paka huyo ni wa aina ya kipekee.

Sauti ya mzee Abilahi Issa Mohamedi

Naye mwenyekiti wa kijiji cha Nangumi, Musa Salumu Nassoro, ameeleza kusikitishwa na tukio hilo, akisema linaweza kujenga taswira mbaya kwa kijiji hicho. Ameongeza kuwa katika kipindi chote cha uongozi wake hajawahi kushuhudia wala kusikia tukio la aina hiyo katika kijiji cha Nangumi.

Sauti ya Musa Salumu Nassoro, mwenyekiti wa kijiji cha Nangumi