

17 February 2025, 20:14 pm
Jamii imekuwa ikiamini kuwa mwanamke au mtoto wa kike hawezi kuwa fundi chuma,Seremala na fundi uashi kama ilivyo kwa mtoto wa kiume hali inayopelekea mwanamke kuwa nyuma katika sekta ya ufundi.
Na Musa Mtepa
Wanaume wa mkoani Mtwara wametakiwa kuwapa nafasi wanawake wao kuendeleza ufundi chuma ili waweze kuwa mafundi, kama ilivyo kwa mafundi wa kiume.
Akizungumza katika mafunzo ya wiki mbili ya kuwajengea uwezo wanawake , yanayofadhiliwa na UNESCO na Al Waleed Philanthropies, yanayojumuisha vijana wa jinsia zote na yanatolewa na Shirika la ADEA Bw Omari Mohamed, mwezeshaji wa mafunzo hayo, amesema wanawake wengi wanakutana na changamoto za kimaadili na kijamii, jambo linalowafanya washindwe kuendeleza fani hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa ADEA, Saidi Chilumba, ameongeza kwamba fani hiyo imekuwa ngumu kwa baadhi ya jamii kwa sababu inachukuliwa kama ya kiume pekee. Hata hivyo, mafunzo hayo yamejumuisha vijana wa kike na wa kiume ambao wamejifunza ufundi chuma kwa nadharia na vitendo, na wameweza kutengeneza vitu mbalimbali vya chuma. Chilumba pia amehimiza vijana hao kubuni bidhaa ndogo zinazohitajika na jamii, ambazo zitakuwa na soko.
Vijana wa kike, Asfa Rashidi na Asha Musa, wameelezea changamoto wanazokutana nazo mtaani, ambapo jamii inawaona kama hawapaswi kufanya kazi zinazochukuliwa kuwa za kiume.
Kwa ujumla, ni juhudi nzuri za kuhakikisha usawa wa kijinsia katika sekta ya ufundi chuma na kuhamasisha wanawake kuchangia katika kukuza uchumi kupitia ufundi.