

17 February 2025, 19:06 pm
Katika misimu miwili iliyopita simba sc haijawahi kushinda mchezo wowote wa ligi kuu katika uwanja wa Majaliwa dhidi ya Timu ya Namungo ,katika michezo miwili waliyocheza katika miimu hiyo miwili wameambulia kupata sare.
Na Musa Mtepa
Timu ya soka ya Simba SC leo Februari 17, 2025, imewasili katika Uwanja wa Ndege wa Mtwara kwa ajili ya kuelekea Ruangwa, mkoani Lindi, ambapo itakutana na timu ya Namungo katika mchezo wa ligi kuu ya NBC Tanzania Bara utakaochezwa Februari 19, 2025.
Meneja wa kitengo cha habari na mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ali, amezungumzia kuhusu maandalizi ya timu kuelekea mchezo huu, akisema kuwa kwa misimu miwili iliyopita, Simba imeshindwa kupata matokeo mazuri dhidi ya Namungo, na hivyo wamejipanga kwa umakini ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mchezo huu.
Aidha, Ahmed Ali akizungumzia kuhusu mbio za ubingwa, amesema kuwa bado ni mapema na tofauti ya pointi kati ya kinara wa ligi na timu zilizopo kwenye nafasi za juu ni ndogo. Hivyo, sare au kupoteza mchezo kunaweza kuondoa timu yoyote katika nafasi yake ya sasa. Simba SC inaendelea kupambana kuhakikisha wanatimiza dhamira yao ya kuwa mabingwa wa msimu huu.
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdala Mwaipaya, ameipongeza klabu ya Simba kwa kuwa timu ya kwanza kutumia usafiri wa ndege wa Air Tanzania kutokea Dar es Salaam hadi Mtwara, baada ya huduma hiyo kurejeshwa rasmi leo, Februari 17, 2025. Mwaipaya amewatakia kila la heri Simba SC kuelekea mchezo wao dhidi ya Namungo utakaochezwa Februari 19, 2025, katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa, Lindi.