Jamii FM
Jamii FM
16 November 2025, 10:08 am

Mkuu wa Wilaya Abdala Mwaipaya amesisitiza uwajibikaji huo kwenye mkutano wa WABISOKO na kuwapongeza wafanyabiashara kwa kudumisha amani na kuwasilisha changamoto zao kwa utulivu. Makamu Mwenyekiti Rashidi Johana amewasilisha maendeleo na changamoto za ushirika.
Na Musa Mtepa
Wajasiriamali wametakiwa kutimiza wajibu wao katika kufanikisha upatikanaji na urejeshaji wa mikopo inayotolewa na serikali kupitia benki washirika, ili kuwezesha watu wengine kunufaika na huduma hiyo.
Kauli hiyo imetolewa Novemba 15, 2025 na Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdala Mwaipaya, wakati wa ufunguzi wa mkutano wa Ushirika wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu Mtwara (WABISOKO) uliofanyika katika viwanja vya Mashujaa, Manispaa ya Mtwara–Mikindani.
Mwaipaya amesema kuwa serikali inatekeleza wajibu wake, lakini ni muhimu kwa wajasiriamali kama walengwa wa mikopo hiyo kuhakikisha wanatimiza masharti na vigezo vinavyohitajika ili kupata na kurejesha mikopo ipasavyo.
Aidha, DC Mwaipaya ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla kwa kudumisha amani na utulivu katika kipindi cha uchaguzi mkuu uliopita. Pia amewapongeza viongozi wa jumuia hiyo kwa kuwa watulivu na kuwasilisha changamoto zao bila kuanzisha vurugu au fujo.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Ushirika wa Wafanyabiashara wa Soko Kuu Mtwara (WABISOKO), Bw. Rashidi Issa Johana, amesema kuwa dhamira kuu ya mkutano huo ni kuwapa wanachama taarifa ya maendeleo tangu viongozi wa sasa walipochukua madaraka, pamoja na changamoto na mafanikio yaliyopatikana.
