Jamii FM

Wanawake wa Mtwara Mikindani Wahimizwa ujiamini katika kupigania nafasi za uongozi

16 November 2024, 17:23 pm

Lulu Abdala Diwani mstaafu viti maalumu Manispaa ya Mtwara Mikindani akizungumza na waandishi wa habari juu ya changamoto za wanawake kushiriki katika uchaguzi(Picha na Musa Mtepa)

November 27,2024 kunatarajiwa kufanyika uchaguzi wa serikali za mitaa ambapo katika kuelekea siku hiyo michakato mbalimbali imeanza kufanyika ikiwemo kujiandikisha katika orodha ya wapiga kura,kuchukua fomu za ushiriki uongozi,kukata na kusikiliza rufaa huku ikisubiriwa tarehe ya kuanza kampeni.

Na Musa Mtepa

Wanawake wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wametakiwa kujiamini na kupambana na wanaume katika kupigania nafasi mbalimbali za uongozi, badala ya kugombea kupitia viti maalumu.

Hayo yamesemwa na Lulu Abdala, Diwani Mstaafu wa Viti Maalumu kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), alipokuwa akifanya mahojiano na Jamii FM Radio tarehe 15 Novemba, 2024.

Katika mahojiano hayo, Lulu Abdala amesisitiza kuwa katika kipindi hiki cha uchaguzi wa serikali za mitaa, wanawake wanapaswa kuwa na moyo wa kujitokeza na kupigania nafasi za uongozi kwa kushindana moja kwa moja na wanaume. Anasema wanawake wanapaswa kuweka nguvu katika vita hii na kujiamini katika mchakato wa kugombea.

Sauti ya 1 Lulu Abdala Diwani mstaafu viti maalumu Manispaa ya Mtwara Mkindani

Lulu pia ameeleza changamoto ambazo wanawake wanakutana nazo hasa katika maeneo ya ukanda wa pwani wa Tanzania, ambapo jamii nyingi bado haijakubaliana na wazo la kuongozwa na mwanamke. Hata hivyo, amewataka wanawake ambao wamejitokeza kugombea nafasi mbalimbali za uongozi katika uchaguzi huu, kukabiliana na changamoto hizo .

Sauti ya 2 Lulu Abdala Diwani mstaafu viti maalumu Manispaa ya Mtwara Mkindani

Lulu Abdala pia amesisitiza kuwa yupo tayari kutoa ushauri na usaidizi kwa wanawake wote, bila kujali chama, dini au kabila zao, katika muktadha wa kuelekea uchaguzi wa serikali za mitaa utakaofanyika tarehe 27 Novemba, 2024.

Sauti ya 3 Lulu Abdala Diwani mstaafu viti maalumu Manispaa ya Mtwara Mkindani

Kauli hii ya Lulu Abdala imekuja wakati ambapo wanawake wengi wanajitokeza kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa, huku akiendelea kuhamasisha wanawake kuwa na umoja na kujitokeza kwa wingi kugombea nafasi za uongozi kwa usawa.