Wadau wa mazingira waiomba TPDC kuendelea usambazaji wa Gesi Asilia majumbani
16 June 2024, 13:48 pm
Gesi inasambazwa majumbani kwa kutumia bomba lakini kwa lengo la kuyafikia masoko ya mbali kutatekelezwa mradi wa LNG Lindi ambapo gesi itabadilishwa na kuwa kimiminika itapakiwa kwenye mitungi mikubwa na ikifika huko itaingizwa kwenye mitambo ya kuibadiliasha kuwa hewa iweze Kwenda kwa watumiaji kwa njia ya mabomba
Na Musa Mtepa
Wadau wa Mazingira mkoani Mtwara wameiomba serikali kupitia shirika la maendeleo la Petroli Tanzania (TPDC) kuharakisha mpango wa matumizi ya nishati safi ya kupikia kupitia Gesi Asilia ili kuondokana na uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi ya kuni na mkaa.
Wadau hao wamesema kuwa Tanzania ni nchi iliyobarikiwa kuwa na Gesi Asilia ya kutosha hivyo ni wakati hivi sasa kwa TPDC kuunga mkono jitihada za Rais Daktari Samia Suluhu Hassani katika matumizi ya nishati safi ya kupikia ili kuepuka matumizi ya nishati chafu ya kupikia inayosababisha kiwango kikubwa katika uharibifu wa Mazingira Pamoja na kuathiri afya ya watumiaji.
Akizungumza Juni 14,2024 wakati wa Warsha ya utoaji Elimu juu ya umuhimu wa sekta ya Mafuta na Gesi kwa wanafunzi wa chuo Stella Maris Mtwara(STEMCO) iliyoandaliwa na chuo hicho chini ya udhamini wa TPDC Stella Masai Mwanamazingira amesema kuwa matumizi ya nishati safi inaweza kutumika kutunza mazingira kwa kiasi kikubwa hivyo ni jukumu la shirika la maendeleo ya Petroli Tanzania kuhakikisha inaendelea na mpango wa usambazaji wa mabomba ya gesi ya kupikia majumbani.
Aidha Stella Masai ametoa wito kwa serikali katika mpango wa matumizi wa nishati safi ya kupikia kutosahau kuwasambazia kwa upande wananchi wa vijijini ambako kwa asilimia kubwa wamekuwa watumiaji wa kuni na mkaa na ndiko athari kubwa ya milipuko ya magonjwa unakotokea.
Kwa upande wake Afisa maendeleo ya jamii kutoka shirika la maendeleo ya Petrol Tanzania Ally Mluge amesema katika kuunga mkono jitihada zinazofanywa na Serikali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania kupitia Rais Daktari Samia Suluhu Hassani TPDC inanafasi kubwa ya kufanya ambako hadi sasa zaidi ya nyumba 1500 zimeunganishwa na gesi asilia huku miradi mingine ikiendelea kufanyika katika maeneo mbalimbali nchini .
Pia Ally Mluge amesema TPDC ina mipango mathubuti ya kuhakikisha kwamba Gesi inasambazwa katika maeneo mbalimbali nchini ili kuwawezesha wananchi pamoja na watumiaji wa nishati hiyo kuweza kupata nafuu ya matumizi wa nishati ya gesi asilia.