TARI Naliendele yatoa elimu ya uvunaji wa ufuta
16 May 2024, 17:46 pm
Wakulima wanashukuru kupitia mbegu zinazozalishwa na kufanyiwa utafiti katika kituo cha Naliendele kwani wamekuwa wakipata tija kwenye uzalishaji hivyo wengine wanakaribishwa kufika na kujifunza namna bora ya uzalishaji wa zao la ufuta.
Na Musa Mtepa
Wakulima na wadau wa ufuta nchini wametakiwa kuzingatia ubora kwa kuanzia katika hatua za awali za kulima, uvunaji na utunzaji wa zao hilo ili kuendana na mahitaji ya soko linavyotaka.
Hayo yamesemwa tarehe 15/5/2024 na mratibu wa programu ya utafiti wa ufuta kitaifa na mtafiti wa zao la ufuta kutoka taasisi ya utafiti wa kilimo (TARI) Naliendele Joseph Mzunda wakati akitoa elimu ya jinsi na namna bora ya kulima na kuvuna kwa baadhi ya wakulima ambapo amesema kuwa wadau wa zao la ufuta lazima waangalie kuwa linapofika mikononi mwao lipo katika hali ya usafi ili kusitokee lawama kutoka kwa wanunuzi.
Aidha Bw Mzunda ameseama kuwa wanunuzi wa ufuta wamekuwa na vigezo maalumu vinavyowafanya kununua ikiwepo ubora,rangi na Ladha yake huku akielezea upekee unaopatikana kwenye ufuta unaozalishwa nchini ukilinganisha na nchi nyingine.
Hata hivyo Bw Joseph Mzunda amewataka wakulima kutunza kiasi cha fedha kwa ajili ya kununua mbegu zilizokuwa bora na kwa ajili ya pembejeo na viuatilifu ili iwasaidie kutumia katika msimu unaofuata wa kilimo cha ufuta
Fatma Athumani na Aisha Wilson ni wakulima wa zao la ufuta kutoka kata ya Naliendele wamesema kupitia elimu waliyoipata kutoka taasisi ya utafiti wa kilimo (TARI) Naliendele itawasaidia katika kuandaa mashamba na namna bora ya kuvuna zao hilo tofauti na hapo awali walivyokuwa wakilima.
Naye Ziada Athumani mkulima wa zao la ufuta kutoka kata ya Naliendele amesema lengo lake lilikuwa kupata elimu ya jinsi gani ya kulima ufuta kwa njia iliyokuwa bora ili aweze kupata tija hivyo kupitia TARI Naliendele amejifunza mengi kiwepo namna ya kupalilia na kuvuna kwake.