Wananchi Mangamba Chini walia na ubovu wa barabara
16 April 2024, 13:03 pm
Barabara hiyo hivi sasa imekuwa Mbovu kupitiliza ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambacho Gari zinazobeba Watoto kuwapeleka shuleni zilikuwa zinapita bila mashaka lakini kwa hivi sasa imekuwa tofauti
Na Grace Hamisi
Wananchi wa mtaa wa Mangamba Chini Manispaa ya Mtwara Mikindani wameiomba serikali kuwaondolea kero ya ubovu wa barabara ya Mangamba -Mkwajuni iliyobomolewa kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha katika mji wa Mtwara .
Wakizungumza na Jamii Fm Radio 13/4/2024 Wananchi hao wamesema kuwa barabara hiyo hivi sasa imekuwa mbovu kupitiliza ukilinganisha na kipindi cha nyuma ambacho gari zinazobeba watoto kuwapeleka shuleni zilikuwa zinapita bila mashaka lakini kwa hivi sasa imekuwa tofauti.
Mohamedi Ali ni mkazi wa Mkwajuni Mangamba Chini ameiomba serikali ya mtaa kutoa taarifa kwa TARURA na kuwashawishi katika kuirekebisha barabara hiyo ili wananchi waweze kuitumia kama hapo awali.
Aidha naye Zamda Dadi Ndumile mkazi wa Mangamba chini amesema kutokana na mvua zinazo nyesha zimetengeneza Korongo hali inayo hatarisha Maisha ya Watoto kwani wakati mwingine wamekuwa wakicheza katika makorongo hayo.
Kwa upande wa Abdala Mtandu Mwenyekiti mtaa wa Mangamba chini amekiri kuwepo kwa changamoto ya Barabara huku akisema kuwa tayari taarifa zimeshafika TARURA na kuahidi wataanza kuifanyia kazi baada ya Msimu wa Mvua kumalizika.
Sambamba na hilo amewaomba Wananchi kuwa na subra katika changamoto hiyo kwani wao kama viongozi wanaendelea kushirikiana na serikali ya kata Pamoja na TARURA katika kuondoa kero hiyo wanayoipitia kwa kipindi hiki.