TPDC yatoa mafunzo kwa wanafunzi wa STEMCO Mtwara
15 June 2024, 15:45 pm
Sekta ya mafuta na gesi ni sekta nyeti ambayo wananchi wengi wanapaswa kufahamu nini kinafanyika huko na miradi gani inatekelezwa hivyo kwa mujibu wa sheria ya mwaka 2015 (Petroleum Act 2015) inaipa TPDC hadhi ya kuwa shirika la mafuta katika utafutaji, usambazaji na uendelezaji
Na Grace Hamisi
Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Juni 14, 2024 limetoa mafunzo kwa wanafunzi wa chuo cha Stella Maris Mtwara (STEMCO) yanaohusiana na mafuta na gesi kwa uchumi endelevu na usalama wa mazingira.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Ofisa Tarafa wa kata ya Ziwani Winifrida Linyembe amesema Tanzania imejaliwa kuwa na gesi asilia ambayo inapatikana mikoa ya Lindi na Mtwara na licha ya kupatikana huo lakini pia imekuwa ikiwanufaisha watanzania kwa ujumla.
Kwa upande wa Afisa maendeleo ya jamii kutoka Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) Ally Mluge amesema kuwa kutoa semina hiyo ni moja ya jitihada za TPDC za kusambaza elimu kuhusu mafuta na gesi asilia kwa makundi mbalimbali lengo ni jamii kuona namna ya matumizi ya gesi asilia yanavyokuwa.
Aidha ameongeza kuwa kukua kwa matumizi ya gesi asilia kunachangia kwa kiasi kikubwa shughuli za maendeleo ya taifa kwani mpaka sasa kwa umeme ambao unaingia kwenye gridi ya taifa zaidi ya asilimia 60 unatokana na gesi asilia.
Kwa upande wa mwanafunzi wa chuoni hapo Petronila Fabian ameshukuru kupata elimu ya namna ya kutumia gesi na kuhifadhi gesi asilia jinsi ilivyo muhimu huku akiiomba TPDC kuwapa nafasi wanafunzi wanaomaliza chuo hapo kushiriki katika kupata elimu ya umuhimu wa matumizi na faida ya Gesi Asilia.