

15 March 2025, 10:59 am
Haya ni mafunzo ya siku moja yaliyohusisha watendaji wa mitaa,viongozi wa dini,wadau na watumiaji wa huduma za maji na Nishati wanaopatikana Manispaa ya Mtwara Mikindani
Na Musa Mtepa
Mamlaka ya Uthibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imeendesha mafunzo kwa watendaji wa mitaa na wadau mbalimbali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kujenga uelewa kuhusu ushirikiano na mamlaka, pamoja na utambuzi wa sheria za mtumiaji na mtoa huduma.
Mafunzo hayo yamefanyika tarehe 14 Machi 2025 katika Hoteli ya Lavilla Nouvelle, iliyopo katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Akifungua mafunzo hayo kwa niaba ya Katibu Tawala wa Mkoa wa Mtwara, Bw. John Luguzya, Katibu Tawala Msaidizi, Sehemu ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu, amewapongeza EWURA kwa kuandaa mafunzo hayo, akieleza kuwa yataongeza uelewa wa masuala ya kiuthibiti, hasa katika sekta za umeme na maji.
Bw. Luguzya amefafanua kuwa, moja ya majukumu ya EWURA ni kuhakikisha huduma za umeme na maji zinapatikana kwa uhakika ili ziweze kuchangia katika ustawi wa uchumi wa nchi.
Meneja wa EWURA Kanda ya Mashariki, Wilfred Mwakalosi, amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia washiriki kuwa katika nafasi nzuri ya kutoa ushauri kwa wananchi kuhusu changamoto zinazojitokeza katika maeneo yao.
Nicolous Mvukie, Afisa Mtendaji wa Mtaa wa Ligula, pamoja na Shehe Mohamed Lidonge, wameeleza kuwa mafunzo hayo yamewaongezea uelewa mkubwa kuhusu masuala ya bili za maji, matumizi ya umeme, na jinsi ya kuchukua hatua pindi wanapokutana na changamoto.
Aidha wamesisitiza kuwa, EWURA inapaswa kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi wa chini kupitia mikutano ya vijiji na mitaa ili kuongeza uelewa juu ya malalamiko yaliyopo katika jamii kuhusu utumiaji wa maji na umeme.