Jamii FM

Mama lishe Mtwara washukuru serikali kusafirisha korosho bandari ya Mtwara

15 February 2025, 15:41 pm

Baadhi ya mama lishe wakiwa katika majukumu yao ya kuhudumia wateja wanaobeba korosho katika Bandari ya Mtwara

Matokeo haya ni baada ya viongozi mbalimbali wa serikali na vyama vya siasa kuipambania Bandari ya Mtwara kuhakikisha inasafirisha Korosho na mazao mengine ili kuinua Uchumi wa mtu mmoja mmoja na mkoa kwa ujumla kama ambavyo msimu wa 2024/25 wa korosho ulivyoshuhudia kuchangamsha mji wa Mtwara.

Na Musa Mtepa

Kitendo cha Mbunge wa Mtwara Mjini, Mhe. Hassani Mtenga, kupigania na kuishawishi Serikali kusafirisha korosho kupitia Bandari ya Mtwara kimepongezwa na wauzaji wa vyakula migahawani, maarufu kama “mama lishe”, kwa kuwasaidia kuongeza kipato chao.

 Zuhura Mmole na Salma Hassani (mama Lulu) wameshukuru hatua hiyo kwa kusema kuwa imesaidia familia zao katika msimu wa mwaka 2024/2025, na wameomba serikali kutumia Bandari ya Mtwara pia kusafirishia mazao na bidhaa mbalimbali ili kusaidia uchumi wa eneo hilo.

Sauti ya Zuhura Mmole na Salma Hassani Mama Lishe

Ahmadi Mohmed Mfanyabiashara mdogo, ameongeza kuwa msimu huu wa 2024/2025 umemletea faida kubwa, akisema kuwa amefanikiwa kuongeza mtaji wake, pia ameomba mazao yanayozalishwa katika mikoa ya Lindi na Mtwara yatumike kupitia bandari hiyo, kwani hiyo itawasaidia vijana kupata fursa za ajira na kujiepusha na vitendo hatarishi vinavyosababishwa na ukosefu wa kazi.

Sauti ya Bw Ahamadi Mohamed mfanyabiashara Mdogo

Johnson Julius, ambaye ni kuli katika Bandari ya Mtwara, ameelezea faida kubwa inayopatikana kwa vijana kujipatia kipato kutokana na korosho kusafirishwa kupitia bandari hiyo.

Sauti ya Johnson Julius mbeba mizigo Bandarini (Kuuli)

Mbunge Mtenga amekuwa mstari wa mbele katika kufuatilia suala hili tangu mwaka 2022, ambapo alihoji kuhusu matumizi ya bandari ya Mtwara kusafirisha korosho. Hii ni baada ya serikali kukamilisha ukarabati wa miundombinu ya bandari hiyo.

Sauti ya Mhe.Hassani Mtenga Mbunge wa Jimbo la Mtwara Mjini

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, alifanya ziara Mtwara Julai 7, 2023, ambapo alikutana na wananchi wa Mtwara katika viwanja vya Bandari ya Mtwara Mikindani na kutoa maagizo kwa wizara kuhakikisha inajiandaa na kupata meli zitakazotumika kusafirisha korosho kutoka bandari hiyo.

Sauti ya Waziri mkuu Kasim Majiliwa akitoa maagizo kwa wizara

Jitihada hizo zimezaa matunda, ambapo msimu wa 2024/2025  korosho zimesafirishwa kupitia Bandari ya Mtwara na kutoa fursa za ajira kwa vijana wa Mtwara, mama lishe, maafisa usafirishaji (bodaboda), pamoja na makuli. Hii imeweza kuongeza kipato cha wananchi mbalimbali kutokana na kazi za kubeba na kusimamia mizigo bandarini.