Jamii FM

AG afanya ziara mkoani Mtwara

14 November 2024, 20:07 pm

Mwanasheria mkuu wa Serikali Hamza S.Johari akiwa katika picha ya pamoja na mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala,mkuu wa wilaya ya Mtwara Abdala Mwaipaya,katibu tawala mkoa wa Mtwara Bi Bahati Geuzye na watendaji wengine wa serikali

Tunaendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo katika ziara hii tunakutana na watumishi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusisitizana juu ya kuwahudumia wananchi.

Na Mwandishi wetu

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mhe. Hamza S. Johari amefanya ziara ya kikazi mkoani Mtwara leo Tarehe 14 Novemba 2024 yenye lengo la kukutana na wadau mbalimbali wa sheria mkoani humo.

Akiwa Mkoani Mtwara, Mhe. Johari amemtembelea Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala, kwa ajili ya kujitambulisha na kumueleza lengo la ziara yake ambayo ni ya kwanza mkoani humo tangu ateuliwe na Mhe.Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kushika nafasi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

Katika salamu zake kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Patrick Sawala amemueleza kuwa Mtwara iko salama, na Serikali inaendelea kushirikia na wadau wengine kuhakikisha kuwa wananchi wanaendelea kuwa salama.

Akielezea lengo la ziara hiyo, Mhe. Johari amesema kuwa ni kutembelea Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Mtwara, na kukutana na watendaji wa ofisi hiyo kwa ajili ya kuimarisha utoaji wa huduma za sheria kwa wananchi.

“Mkoa wa Mtwara ni mkubwa na una shughuli nyingi za kiuchumi, hivyo ni vema kuwa na mawasiliano ya karibu kati ya Ofisi ya AG ofisi ya Mkuu wa Mkoa na wananchi wengine”

“kama nilivyosema tunaendelea kuimarisha utoaji wa huduma kwa wananchi katika maeneo mbalimbali nchini, hivyo katika ziara hii tunakutana na watumishi wa ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kusisitizana juu ya kuwahudumia wananchi” ameeleza Mhe. Johari.

Mwanasheria Mkuu wa Serikali pia ametembelea eneo linalotarajiwa kujengwa jengo la Ofisi za Kanda, pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mkoa wa Mtwara, iliyopo jengo la Chama cha Waalimu Mkoa wa Mtwara.