Jamii FM
Jamii FM
14 August 2025, 12:53 pm

Zaidi ya matukio 1,338 ya ukatili yameripotiwa Mtwara ndani ya miezi sita, huku Nanyumbu na Tandahimba zikiongoza. Viongozi wa ustawi wa jamii na dini watoa sababu, mikakati na wito wa kuimarisha malezi na maadili.
Na Musa Mtepa
Zaidi ya matukio 1,338 ya ukatili yameripotiwa katika kipindi cha miezi sita iliyopita mkoani Mtwara, huku wilaya za Nanyumbu na Tandahimba zikiongoza kwa idadi kubwa ya matukio hayo.
Akizungumza baada ya kongamano lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara kwa kushirikiana na wadau wa mradi wa Mtoto Kwanza, unaochagizwa na Programu ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto, Mtandao wa Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto (TECDEN) na asasi ya KIMAS, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Mtwara, Theresia Ngonyani, amesema kuwa kuanzia mwezi Januari hadi Juni mwaka huu, jumla ya matukio 1,338 ya ukatili yameripotiwa.
Kati ya matukio hayo, 1,100 yalihusu watoto na 238 yalihusu watu wazima. Aidha, visa vya ukatili wa kingono kwa Watoto vilikuwa 202, huku wilaya ya Nanyumbu ikiongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya matukio hayo.

Akizungumzia hali hiyo, Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya ya Nanyumbu, Johari Rashidi, amesema kuwa sababu kubwa zinazochangia ukatili katika wilaya hiyo ni pamoja na ukosefu wa elimu ya kijinsia na umasikini uliokithiri katika familia nyingi.
Ameongeza kuwa mikakati iliyopo ni pamoja na kuendelea kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia na watoto, pamoja na kuwaunganisha waathirika na taasisi mbalimbali za kiraia ili kuwasaidia kupata huduma na msaada unaohitajika.
Kwa upande wao, viongozi wa dini wamesema kuwa ili kupunguza vitendo vya ukatili na mmomonyoko wa maadili, jamii inapaswa kuwekeza nguvu katika kumjua Mungu na kutambua mafunzo na misingi ya imani zao.
