RC Sawala ashuhudia utiaji saini kongani la viwanda Maranje Mtwara
14 June 2024, 21:11 pm
Kusainiwa kwa makataba huu kati ya Bodi ya KoroshoTanzania (CBT) na mkandarasi na kampuni ya Malagarasi Enterprises and Contractors Limited ni mwanzo wa CBT kumiliki viwanda vya pqmoja vya kubangua korosho na kusindika bidhaa zake ambapo uendeshaji wa viwanda hivi vitahusisha serikali na sekta binafsi.
Na Msafiri Kipila
Mkuu wa mkoa wa Mtwara Kanali Patrick Sawala ameipongeza bodi ya Korosho Tanzania (CBT) kwa kuharakisha mchakato wa ujenzi wa kongani la viwanda huku akitoa wito kwa mkandarasi kuzingatia Masharti ya mkataba ikiwemo utunzaji wa Mazingira.
Akizungumza leo Juni 14,2024 kwenye hafla ya utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Maghala mawili ya kuhifadhia korosho katika kijiji cha Maranje Halmashauri ya mji Nanyamba kati ya Bodi ya Korosho Tanzania na kampuni ya Malagarasi Interprises and Contractors limited RC Sawala ameipongeza Bodi hiyo kwa kutekeleza kwa haraka yale wanayokubaliana katika vikao kwa manufaa ya Wakulima wa korosho na wananchi kwa ujumla.
Aidha Mkuu wa mkoa Kanali Patrick Sawala ametoa wito kwa pande zote mbili zilizotiliana Saini kuzingatia matakwa ya mkataba kwa kujenga Maghala hayo katika ubora wa hali ya juu kwa kuzingatia thamani halisi ya fedha pamoja na kujenga kwa muda uliopangwa.
katika hatua nyingine Mkuu wa mkoa amemtaka mkandarasi kutoa ajira kwa watu wa maeneo ya karibu kwa zile kazi ambazo wanauwezo wa kuzifanya ili nao wawe sehemu ya mradi huo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Bodi ya Korosho Tanzania Brig Generali Mstaafu Aloyce Mwanjile amesema kuwa ujenzi huo ni katika kutekeleza mradi wa ujenzi wa kongani ya viwanda katika eneo la Maranje lenye ukubwa hekari 1572.
Dadi Tindo na fadina Mmogo Wananchi wa Kijiji cha Maranje wamefurahishwa uwepo mradi wa kongani la Viwanda katika eneo hilo huku wakimuomba mkandarasi kuhakikisha wanatoa ajira kwa wakazi maeneo hayo ili nao waweze kunufaika na uwepo wa viwanda hivyo.