Wadau waombwa kusaidia ujenzi wa ghala la kijiji Mtwara
14 May 2024, 08:24 am
Tumeamua kujenga ghala hili kwasababu Kijiji chetu hatuna ghara na mazao yetu sasa hivi tumekua tukiazima jengo la maarifa ya kilimo la kata ambalo tumekuwa tukilitumia kupimia kwa kila pale inapofikia msimu wa korosho na ufuta tukaona bora tujichange ili tujenge ghara la kwetu wenyewe.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa kijiji cha Imekuwa kata ya Naumbu halmashauri ya Mtwara Vijijini mkoani Mtwara wameomba wadau wa maendeleo kujitokeza katika kutoa msaada wa hali na mali katika ujenzi wa Ghala la Kijiji linalo kadiliwa kuwa na thamani ya zaidi ya shilingi milioni 80 linalojengwa kwa nguvu za wananchi.
Akizungumza na jamii fm Radio tarehe 11/5/2024 Issa Tikitiki mwananchi wa Kijiji hicho amesema kuwa wamekuwa na kero ya Ghala ya kuhifadhia na kuuza mazao kwa muda mrefu hali iliyowafanya kukubaliana na kuanza ujenzi kupitia nguvu za wananchi huku ikiwa imefikia hatua ya msingi katika ujenzi huo.
Mwenyekiti wa kamati ya ujenzi wa Ghala hilo Bw Ahamadi Mfaume Alawi amesema ujenzi umefikia katika hatua ya msingi ambayo haijakamilika na bado kukiwa na upungufu wa vifaa vya kukamilishia ujenzi huo ambapo amevitaja kuwa ni Pamoja na Saruji,Kokoto ,Mchanga na nondo.
Aidha Bw Alawi amesema uhitaji wa ujenzi wa ghala katika Kijiji hicho ni mkubwa kutokana na kuwepo kwa wakulima wengi wa zao la korosho na ufuta ambao wamekuwa wakipata shida wakati wa kuhifadhi na kuuza mazao hayo .
Naye fundi Mkuu wa ujenzi wa mradio huo Juma Bakari Singa amesema kama vifaa vingekuwepo na kutokana na mafundi wasaidizi kuwa wengi ndani ya mwezi mmoja wangeweza kukamilisha ujenzi wa boma la Ghala hilo .
Kwa upande wake mwenyekiti wa Kijiji cha Imekuwa Bw Mathayo Mwanga (Mmungulange) amesema ujenzi wa ghala hilo limetokana na makubaliano ya wananchi waliyofikia katika mikutano mikuu ya kijiji ambapo wananchi walikubaliana kuchangia shilingi 50 kwa kila kilo moja ya Korosho na ufuta yanapopelekwa sokoni.
Pia Mwenyekiti amesema katika michango hiyo walifanikiwa kupata fedha zaidi ya shilingi milioni 3 ambazo zimesadia kufikia katika hatua hiyo Pamoja na michango kutoka kwa viongozi mbalimbali wa kisiasa akiwemo Mbunge wa jimbo la Mtwara vijijini Shamsia Azizi Mtamba ambae alitoa mifuko 70 ya saruji Pamoja na Nondo 45 huku Diwani wa kata ya Mayanga akitoa mifuko 20 ya saruji.