Jamii FM
Jamii FM
13 July 2025, 12:33 pm

Wakulima wa Kijiji cha Kilambo, wameiomba Serikali kusaidia kudhibiti viboko wanaovamia na kuharibu mazao yao usiku katika ukanda wa Mto Ruvuma, wakitumia njia hatarishi kujilinda. Wanaomba msaada wa magemu skauti ili kulinda maisha na mazao yao.
Na Musa Mtepa
Wakulima wa mazao ya msimu kutoka Kijiji cha Kilambo, kilichopo ukanda wa Mto Ruvuma, wameiomba Serikali kupitia Mamlaka ya Wanyamapori kuwasaidia kudhibiti viboko wanaovamia mashamba yao na kuharibu mazao kila usiku.
Wakizungumza na Jamii FM Radio, wakulima hao wamesema wamekuwa wakipata usumbufu mkubwa hasa nyakati za usiku, ambapo viboko huingia mashambani kuanzia saa 12 jioni hadi saa 8 usiku. Wamesema wamekuwa wakilazimika kutumia mawe, magongo, mwanga wa tochi na hata kuwasha moto kuwafukuza viboko hao – njia ambazo ni hatarishi kwa maisha yao.
Charles Kalamu na Mohamedi Selemani, wakulima wa kunde na mahindi, wanasema viboko hao wamekuwa chanzo kikubwa cha uharibifu wa mazao yao kwa siku nyingi sasa.
Kwa upande wake, Rabia Mohamedi, mkulima wa mazao ya kunde, amesema kuwa licha ya juhudi zao, hali bado ni mbaya na wanahitaji msaada wa kitaalamu.

Wakulima wameiomba Serikali kupitia taasisi kama TAWA na TANAPA kupeleka magemu skauti wa kudumu katika eneo hilo ili kulinda maisha ya wananchi na usalama wa mazao yao.
Mwenyekiti mstaafu wa kitongoji cha Misufini, Bw. Mfaume Hamisi Amri, amethibitisha kuwepo kwa kero hiyo kwa muda mrefu na kusema kuwa zaidi ya hekta 10 za mashamba tayari zimeharibiwa.
