Madiwani halmashauri ya Kilindi wajifunza uzalishaji wa Korosho TARI Naliendele
13 June 2024, 19:00 pm
Baada ya kikao kilichoagiza kila halmashauri kuwa na vyanzo vipya vya mapato halmashauri ya Kilindi ilifikiria kuwa zao la korosho linaweza kuwa chanzo sahihi cha kuongeza mapato kwa siku za usoni hasa hamasa ikitolewa kwa wananchi na ukizingatia kuna misitu mingi ambayo haijafanyiwa kazi.
Na Musa Mtepa
Kamati ya fedha, Uongozi na Mipango ya halmashauri ya wilaya ya kilindi mkoani Tanga Juni 12,2024 wamefanya ziara ya siku moja katika kituo cha utafiti wa kilimo (TARI) Naliendele kujifunza taratibu za Miche na Mbegu ,Ubora na Magonjwa yanayoweza kukabiri zao la korosho na namna ya kuyaondoa.
Akizungumza baada ya ziara hiyo Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Kilindi Idrisa Omari Mgaza amesema wamefika mkoani Mtwara kwa dhamira ya kujifunza juu ya kilimo cha zao la Korosho ikiwa ni moja ya mpango wa kuongeza mapato ya halmashauri kupitia zao hilo .
Aidha Mh Mgaza amesema mkoa wa Tanga wanalima Korosho ila sio kwa kiwango kikubwa kama ilivyo katika mkoa wa Mtwara na wao kama halmashauri kwa mwaka huu wakitarajia kuanzia kulima hekari 400 za Mikorosho.
Seiya Keiya na Michael Yeyo wajumbe wa kamati ya fedha ,uongozi na mipango kutoka halmashauri ya Kilindi wamesema ziara hiyo ni mojawapo ya kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha kila halmashauri kuwa na vyanzo vipya vya mapato .
Akimwakilisha mkurugenzi mtendaji mkuu wa Idara ya kilimo, Mifugo na uvuvi wa halmashauri ya Kilindi Godian Gwiago amesema wamekuwa wakihangaika kwa muda mrefu katika kuongeza mapato ya halmashauri hivyo baada ya kushauriana kupitia baraza la Madiwani wakapitisha rasmi kilimo cha zao la korosho ili litumike kuongeza mapato hayo kwa siku za usoni.
Kwa upande wake Bakari Kidunda mtafiti ambae pia kaimu mkurugenzi wa kituo cha utafit wa kilimo TARI Naliendele amesema dhamira kubwa ya ujio wao ni kujifunza na kupata uelewa juu ya kilimo bora cha zao la korosho Pamoja na fursa zake
Pamoja na hayo kaimu Mkurugenzi ameelezea sababu zinazosababisha kutembelewa na wageni kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi kuwa ni Pamoja na kuwepo kwa watafiti wenye ujuzi na kujitangaza kazi zinazofanyika kituoni hapo .