Jamii FM

Mashamba 15 yashambuliwa na viboko Mnuyo

13 April 2026, 12:24

Sehemu ya mashamba ya wakulima wa kijiji cha Mnuyo kata ya Msimbati yaliyoshambuliwa na Viboko (Picha na Musa Mtepa)

Wananchi wa kijiji cha Mnuyo mkoani Mtwara wamelalamikia mashambulizi ya viboko mashambani, wakiiomba serikali kuchukua hatua za haraka kuwalinda na kuzuia hatari ya baa la njaa.

Na Musa Mtepa

Wananchi wa Kijiji cha Mnuyo, kata ya Msimbati, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, mkoani Mtwara, wameiomba serikali kupitia mamlaka zinazohusika na wanyamapori kufika kijijini hapo ili kuwaondolea changamoto ya wanyama aina ya viboko wanaoshambulia mashamba yao ya mpunga.

Wakizungumza na Jamii FM Redio Aprili 10,2026, wananchi hao wamesema kuwa katika siku za hivi karibuni wamekuwa wakikumbwa na changamoto kubwa ya viboko kuvamia mashamba yao ya mpunga nyakati za usiku, hali inayowatishia baa la njaa siku za usoni.

Sauti ya wakulima wa mpunga Kijiji cha Mnuyo

Aidha, wananchi hao wameiomba serikali kuwasaidia kwa haraka kutatua changamoto hiyo, ambayo imekuwa kubwa kwao kiasi cha baadhi yao kukata tamaa ya kuendelea na shughuli za kilimo kutokana na uwepo wa wanyama hao.

Sauti ya wakulima wa mpunga Kijiji cha Mnuyo
Kinyesi cha Mnyama Boko kikionekana pembezoni mwa shamba la Mpunga (Picha na Musa Mtepa)

Kwa upande wake, mwenyekiti wa Kijiji cha Mnuyo, Yusuf Salumu, amekiri kupokea taarifa za uwepo wa wanyama hao katika eneo hilo, akisema tayari amezifikisha katika Halmashauri ya Wilaya kwa ajili ya hatua zaidi.

Aidha, mwenyekiti huyo amesema viboko hao wanaotoka Mto Ruvuma wameshashambulia mashamba 15 ya wakulima wa kijiji hicho, huku akiomba mamlaka zinazohusika na wanyamapori kuchukua hatua za haraka kuwaondoa wanyama hao.

Sauti ya Yusuf Salumu, mwenyekiti wa Kijiji cha Mnuyo