

13 March 2025, 21:19 pm
Msaada ulioletwa na Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wadau umejumuisha vifaa mbalimbali ikiwemo unga wa sembe, dona, mchele, sukari, mafuta ya kupikia, sabuni za unga, chumvi, sabuni za kuogea, taulo za kike, magodoro, blanketi, vyandarua, nepi za kisasa (diapers), sahani, ndoo za lita 20 na 10, madumu pamoja na mikeka.
Na Musa Mtepa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanal Patrick Sawala, amekabidhi rasmi vifaa vya maafa kwa Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Mhe. Abdallah Mwaipaya kwa ajili ya kugawa kwa waathirika wa maafa yaliyosababishwa na mvua kubwa zilizonyesha kuanzia tarehe 3 hadi 7 Februari 2025.
Hafla ya kukabidhi vifaa hivyo ilifanyika leo Machi 13, 2025, katika viwanja vya ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mtwara.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa, Kanal Sawala, ametoa shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kupitia ofisi ya Waziri Mkuu, pamoja na wadau wote waliochangia vifaa hivyo ili kuwafariji waathirika wa mafuriko.
Pia, Kanal Sawala ametoa rai kwa wananchi wa Mtwara kuhakikisha nyumba zao wanapojenga zinakuwa na uimara ili kupunguza athari za mafuriko ya baadaye.
Aidha RC Sawala amesema kuwa, serikali itaendelea kufanya marekebisho ya miundombinu iliyoharibika kutokana na mvua hizo kupitia miradi mbalimbali, kama vile TACTIC, ili kuepusha maafa kama hayo siku zijazo.
Kwa upande wake, Juma Napinda, Afisa Mtendaji kutoka TCCIA Mkoa wa Mtwara, kama mdau ameguswa na maafa kwa kiasi kikubwa kwasababu waliopata madhira ni wadau wao ambao pia ni Wananchi wa mkoa wa Mtwara ambao kwa namna moja ua nyingine wanapaswa kusaidia ili kuwawezesha kurudi katika maisha yao ya kila siku.
Mbwana Ahmedi, Meneja wa Benki ya CRDB Tawi la Mtwara, ameeleza kuwa benki hiyo pia imeshirikiana na serikali na wadau wengine ili kuhakikisha usalama wa wananchi na kutoa msaada kwa wahanga wa mafuriko.
Juma Chijinga, Diwani wa Kata ya Chuno, ameishukuru serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa juhudi zake za kusaidia wananchi wa Mtwara pamoja na kusema kuwa serikali ina mipango mizuri ya kuhakikisha kero za mafuriko zinazotokana na mvua zitapatiwa suluhu kupitia miradi ya TACTIC.
Chijinga ametoa wito kwa serikali na wadau kujitahidi kutibu maji yaliyotuama katika maeneo mbalimbali ya Manispaa ya Mtwara Mikindani, ili kuepuka magonjwa kama vile malaria na kipindupindu yanayotokana na maji hayo.