Diwani Namtumbuka afanya kikao kazi na viongozi wa vijiji, vitongoji
11 December 2024, 00:17 am
Hiki ni kikao kazi kilichoitishwa na Diwani wa kata ya Namtumbuka Al-hajji Salumu Lipwelele chenye lengo la kutambuana na kufahamishana majukumu mbalimbali kwa viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na wataalamu wa Idara mbalimbali katika kata hiyo.
Na Musa Mtepa
Leo, Disemba 10, 2024, Diwani wa Kata ya Namtumbuka, Al-hajji Salumu Lipwelele, amefanya kikao kazi na viongozi wa vijiji na vitongoji vinavyopatikana katika kata hiyo. Lengo kuu la kikao hicho lilikuwa ni kutambuana na kujua majukumu ya kila kiongozi katika utekelezaji wa shughuli zao za maendeleo.
Akizungumza katika kikao hicho, Al-hajji Lipwelele amesisitiza kuwa kutokana na imani kubwa iliyojitokeza kutoka kwa wananchi katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Novemba 27, 2024, ambapo viongozi wote wa chama cha Mapinduzi (CCM) walichaguliwa, ni muhimu kwa viongozi hao kukutana, wakuu wa idara, na kufahamiana ili kuhakikisha utekelezaji wa majukumu yao unaenda kwa ufanisi.
Alhajji Lipwelele amewataka wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuwa viongozi wa kweli na kusimamia maendeleo ya kata ya Namtumbuka katika miradi ya maendeleo inayotekelezwa na pia kutoa taarifa za maendeleo kwa ngazi ya vijiji na vitongoji. Amesisitiza ushirikiano wa karibu kati ya viongozi na Idara za Serikali ili kufanikisha maendeleo kwa haraka.
Vilevile, ametoa wito kwa wataalamu wa idara mbalimbali kushuka hadi ngazi za chini na kutoa elimu kwa wananchi kuhusu namna idara zao zinavyofanya kazi, ili kuimarisha ushirikiano katika utekelezaji wa majukumu yao.
Kwa upande wa maafisa kilimo na mifugo, wamempongeza Diwani Lipwelele kwa jitihada zake za kuandaa kikao hicho na wamesisitiza umuhimu wa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao.
Naye, Mwalimu Masumbuko Richard, Afisa Elimu wa Kata ya Namtumbuka, amezungumzia suala la utoro wa wanafunzi katika elimu ya sekondari kwa kusisitiza kuwa viongozi wa vijiji wanapaswa kujitokeza na kuzungumza na wazazi kuhusu umuhimu wa kutokomeza utoro .
Baadhi ya viongozi wa vijiji na vitongoji wamekubaliana na maelekezo hayo na kumpongeza Diwani kwa kuandaa kikao hicho pamoja na kuahidi kutekeleza yote yaliyozungumzwa na kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kuboresha maendeleo ya kata ya Namtumbuka.