Jamii FM

‘Sauti ya mwanamke’ kunufaisha wananchi 13,500 Mtwara

11 February 2025, 14:36 pm

Afisa ufuatiliaji wa Nerio Paralegal Mtwara Bi Judith Chitanda akielezea jinsi mradi utakavyotekelezwa katika Manispaa ya Mtwara Mkindani(Picha na Musa Mtepa)

Mradi huu unatarajia kutekelezwa katika kata zote 18 za manispaa ya Mtwara Mikindani huku lengo kuu likiwa kutoa elimu juu ya msaada wa kisheria ,haki na umiliki wa mali (Ardhi) na unyanyasaji wa kijinsia

Na Musa Mtepa

Zaidi ya wananchi 13,000 wa Manispaa ya Mtwara Mikindani wanatarajiwa kunufaika na mradi wa “Sauti ya Mwanamke”, ambao unalenga kufikia jamii yenye usawa, hususani wanawake, na kutoa elimu kuhusu masuala ya kisheria na ukatili wa kijinsia. Mradi huu unakusudia kuelimisha jamii juu ya haki za wanawake na watoto, na kuhamasisha kupinga vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika jamii.

Akizungumza baada ya kuutambulisha mradi huo kwa viongozi wa serikali na wadau wa maendeleo ya jamii, Bi. Judith Chitanda, Afisa Tathmini na Ufuatiliaji kutoka shirika lisilo la kiserikali la Nerio Paralegal Mtwara, amesema mradi huo unatarajiwa kufikia zaidi ya watu 13,000, huku walengwa wakuu wakiwa wanawake na watoto, ambao mara nyingi wamekuwa wahanga wa vitendo vya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia.

Sauti ya 1 Bi Judith Chitanda afisa ufuatiliaji Nerio Paralegal Mtwara

Bi. Chitanda ametoa wito kwa wanawake kujitokeza kwa wingi katika utekelezaji wa utoaji elimu katika kata zao ili waweze kupata elimu ya masuala ya kisheria na kuondoa hali ya unyanyasaji wa kijinsia.

Sauti ya 2 Bi Judith Chitanda afisa ufuatiliaji Nerio Paralegal Mtwara

Kwa upande wake, Saidi Ismail, Mratibu wa Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake na Watoto Mtwara Mjini cha Nerio, amesema kuwa mradi wa “Sauti ya Mwanamke” unalenga kumuinua mtoto wa kike na makundi maalumu kwa kipindi cha miezi 12. Pia amesisitiza kuwa mradi huu utajumuisha wadau mbalimbali, wakiwemo watendaji wa kata, madiwani, viongozi wa mashirika yasiyo ya kiserikali, na watu wa ustawi na maendeleo ya jamii, ambapo dhamira kuu ni kuhakikisha kwamba wote wanahusika katika utekelezaji wa mradi huo.

Sauti ya Saidi Ismail Mratibu wa Nerio Paralegal Mtwara
Saidi Ismail Mratibu wa Nerio Paralegal Mtwara

Viongozi wa kata na wadau wa maendeleo ya jamii wameupokea mradi kwa mikono miwili na wametoa wito kwa wananchi, hasa wanawake, kujitokeza kwa wingi ili waweze kutambua haki zao kupitia msaada wa kisheria na elimu ya kupambana na unyanyasaji wa kijinsia.

Sauti ya wadau wa viongozi wa kata