Jamii FM

DC Mtwara azindua uchaguzi Ndile Cup

10 November 2024, 08:44 am

Mkuu wa Wialaya ya Mtwara ,Abdala Mwaipaya akikagua timu wakati wa ufunguzi wa Uchaguzi Ndile Cup katika uwanja wa Titanic uliopo Mikindani Manispaa ya Mtwara Mkindani(Picha na Musa Mtepa)

Huu ni msimu wanne wa  mashindano hayo ambayo yamekuwa yakijigeuza kila mwaka kutokana na matukio makubwa ya kitaifa   ambapo mwaka 2022 yalitwa Sensa Ndile Cup na mwaka yanajulikana na kama Uchaguzi Ndile Cup.

Na Musa Mtepa

Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, Abdala Mwaipaya, amezindua rasmi mashindano ya mpira wa miguu ya Uchaguzi Ndile Cup tarehe 9 Novemba 2024.

Mashindano hayo yana lengo la kuhamasisha ushiriki wa wananchi, hasa vijana, katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika Manispaa ya Mtwara Mikindani.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mwaipaya ameeleza furaha yake kwa juhudi za Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani, Shadida Ndile, kwa kuwaunganisha vijana kupitia michezo, jambo linaloisaidia jamii kwa kuwaleta pamoja, kuimarisha afya na kuzuia vijana kushiriki katika shughuli zisizo za kisheria.

Sauti ya 1 Abdala Mwaipaya mkuu wa wilaya ya Mtwara

Aidha, ametoa wito kwa wanamichezo na wananchi kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika uchaguzi wa serikali za mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 27 Novemba 2024 na kuwasisitiza kuwa ni haki ya kikatiba ya kila raia kupiga kura na kuchagua viongozi wao.

Sauti ya 2 Abdala Mwaipaya mkuu wa wilaya ya Mtwara

Meya Shadida Ndile ameeleza kuwa lengo la ligi hiyo ni kuhakikisha wananchi, hasa vijana, wanahamasishwa na kushiriki kwa wingi katika uchaguzi.

Amesema kuwa kwa vijana kushiriki michezoni, wanapata fursa ya kuwa na umoja, kufanya mazoezi na kuwa na afya bora, jambo ambalo linawawezesha kuwa na nguvu ya kujitokeza kwa wingi kupiga kura siku ya uchaguzi.

Sauti ya Shadida Ndile Mstahiki meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Mtwara Mikindani akizungumza na wanamichezo kwenye uzinduzi wa Uchaguzi Ndile Cup(Picha na Musa Mtepa

Kassim Ngumbi, Mratibu wa mashindano ya Uchaguzi Ndile Cup, amefafanua kuwa mashindano hayo yatashirikisha jumla ya timu 18 kutoka kila kata za Manispaa ya Mtwara Mikindani na mshindi wa mashindano atapata zawadi ya shilingi Milioni moja (1,000,000/=), wakati mshindi wa pili atajinyakulia shilingi Laki tano (500,000/=).

Sauti ya Kassim Ngumbi Mratibu wa Uchaguzi Ndile Cup

Mashindano haya yanaendelea kuwa na umuhimu mkubwa katika kuhamasisha jamii kwa ujumla kushiriki katika shughuli za kijamii na za kisiasa, huku vijana wakiwa ni wadau wakubwa katika mchakato huu.