Jamii FM
Jamii FM
9 December 2025, 12:25 pm

Afisa wa TASA, imeitaka jamii kutenga muda wa kufikiria na kutoa maamuzi sahihi katika kutatua migogoro, ikisisitiza kuepuka hisia na kutoegemea upande wowote
Na Musa Mtepa
Jamii imetakiwa kutenga muda wa kufikiria, kuchakata na kutoa maamuzi sahihi katika kutatua migogoro inayowakabili katika maeneo yao.
Hayo yamesemwa na Afisa Tathmini na ufuatiliaji kutoka shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Safety Alliance (TASA) linalofanya kazi katika Manispaa ya Mtwara–Mikindani, Hamisi Rashidi Mwinshekhe, kupitia kipindi cha Dira ya Asubuhi kinachorushwa na kituo cha redio cha Jamii FM Mtwara.
Amesema kuwa mgogoro ni hali ya kuwepo kwa mivutano ya kimawazo au kimtazamo, hivyo ni muhimu jamii kutenga muda wa kutosha wakati wa mchakato wa utatuzi ili kuhakikisha kila upande unaridhika na maamuzi yatakayofikiwa.
Aidha, Mwinshekhe amesema kuwa kumekuwa na sababu mbalimbali zinazosababisha kuibuka kwa migogoro katika jamii, ambazo kwa namna moja au nyingine ni muhimu kuepukika ili kujenga jamii imara na yenye amani.
Ameongeza kuwa kuna mambo muhimu ya kuzingatia wakati wa kutatua migogoro, ikiwemo kuepuka matumizi ya hisia, kuonesha huruma, pamoja na kutoegemea upande wowote katika mgogoro unaoendelea.
Shirika la TASA kwa sasa linatekeleza mradi wa “Amani Yetu, Kesho Yetu” katika kata tano za Halmashauri ya Mtwara Vijijini, ambazo ni Nalingu, Madimba, Msimbati, Tangazo na Mahurunga.
Mradi huu unalenga kuelimisha jamii, hususan vijana, kuhusu athari za uvunjifu wa amani na umuhimu wa kudumisha utulivu katika maeneo yao.