Jamii FM
Jamii FM
9 January 2026, 09:27 am

Mkuu wa Mkoa wa Mtwara ameitaka TANROADS kuongeza usimamizi kwa mkandarasi wa barabara ya Mnivata–Masasi baada ya mradi kusuasua. TANROADS imesema chanzo ni mkandarasi na hatua tayari zimechukuliwa kuharakisha ujenzi
Na Musa Mtepa
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Patrick Sawala, ameitaka Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Mtwara kuendelea kumsimamia kikamilifu mkandarasi anayetekeleza mradi wa ujenzi wa barabara ya uchumi ya Mnivata–Tandahimba–Newala–Masasi yenye urefu wa kilomita 160 kwa kiwango cha lami, ili kuhakikisha unakamilika kwa wakati na kwa kuzingatia ubora unaotakiwa.
Kanali Sawala ametoa maelekezo hayo Januari 8, 2026, wakati wa kikao cha Bodi ya Barabara Mkoa wa Mtwara kwa mwaka wa fedha 2024/2025 na 2025/2026, kilichofanyika katika ukumbi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Kanda ya Mtwara, Manispaa ya Mtwara Mikindani.
Amesema utekelezaji wa mradi huo haujaenda kwa kasi ya kuridhisha, hali iliyomlazimu kuielekeza TANROADS kuongeza usimamizi kwa mkandarasi ili kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ufanisi na kwa muda uliopangwa.

Kwa upande wao, Mbunge wa Jimbo la Nanyamba, Abdaa Dadi Chikota, pamoja na Mwenyekiti wa Halmashauri ya Newala, Yusuf Kateule, wamehoji changamoto halisi inayomkabili mkandarasi huyo, wakitaka kufahamu iwapo kuchelewa kwa mradi kunasababishwa na ukosefu wa fedha au uzembe wa mkandarasi mwenyewe.

Akizungumzia kusuasua kwa mradi huo, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Mtwara, Emil Zengo, amesema tayari wamemwondoa msimamizi mkuu wa mkandarasi na kumleta msimamizi mwingine, ikiwa ni sehemu ya hatua za kuharakisha utekelezaji wa ujenzi wa barabara hiyo.
Aidha, amesema kuwa kuhusu ujenzi wa barabara za mchepuko, amemuelekeza mhandisi mshauri kumkata mkandarasi malipo yanayohusiana na kazi ambazo hazijatekelezwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Akijibu maswali kutoka kwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Newala na Mbunge wa Nanyamba kuhusu iwapo chanzo cha kusuasua kwa mradi huo ni fedha au mkandarasi, Meneja wa TANROADS amesema chanzo kikuu ni mkandarasi, huku akisisitiza kuwa hatua stahiki tayari zimechukuliwa kurekebisha hali hiyo.
Kwa upande wake, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mtwara, Ibrahim Mjanakheri Ibrahim, akizungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa Chama hicho Mkoa, amesema CCM inaunga mkono azimio la kuitaka TANROADS kuharakisha kwa kasi zaidi ujenzi wa barabara hiyo ya uchumi kutokana na umuhimu wake katika kuchochea maendeleo ya wananchi wa Mkoa wa Mtwara.
