Jamii FM
Jamii FM
8 December 2025, 11:14 am

Serikali imeombwa kuongeza wanunuzi wa zao la mwani ili kuboresha ushindani wa soko huku wakulima wakilalamikia bei ya shilingi 800 ambayo haiendani na gharama za uzalishaji na usafirishaji kutoka baharini
Na Musa Mtepa
Wakulima wa mwani kutoka Kijiji cha Naumbu, Kata ya Naumbu, Halmashauri ya Mtwara Vijijini wameiomba Serikali pamoja na wadau wa zao hilo kuhakikisha kunakuwepo na ongezeko la wanunuzi ili kuongeza ushindani wa soko.
Wakizungumza na Jamii FM Radio , wakulima hao wamesema kuwa bei ya mwani inayofikia shilingi 800 kwa kilo haiendani na gharama pamoja na mahitaji yao ukilinganisha na uzalishaji wanaoufanya.
Wamesisitiza kuwa ongezeko la wanunuzi litaongeza ushindani na hivyo kusaidia kupandisha bei ili waweze kunufaika zaidi na zao hilo.
Aidha, wameeleza kuwa ili kuzalisha na kufikisha mwani nchi kavu, hulazimika kugharamia usafirishaji kutoka baharini, hivyo kwa bei ya shilingi 800 kwa kilo hawawezi kupata kipato kinachokidhi mahitaji yao.
Akizungumzia hali ya uzalishaji wa mwani katika kijiji hicho, mkulima Bi Bibie Ali Kitenge amesema kuwa wamekuwa wazalishaji wakubwa wa zao hilo, huku wakizalisha kila baada ya siku 45.
Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Naumbu Kusini, Bw. Selemani Shineni, amesema soko la mwani bado ni changamoto kubwa, hali inayosababisha kupokea malalamiko mengi kutoka kwa wakulima wanaoomba watafutiwe soko lenye tija.
Aidha, Shineni ameiomba halmashauri, kupitia maafisa uvuvi, kutowazuia wanunuzi wengine wanaojitokeza kununua mwani. Amesema kuwa kama kuna vigezo wanunuzi wanashindwa kuvifuata, wanapaswa kuelezwa ili wavifuate na hatimaye waweze kununua, jambo litakalowezesha wakulima kunufaika na zao lao.
