Jamii FM

Madiwani Mtwara wasusia baraza kisa matukio ya uchaguzi wa serikali za mitaa

8 November 2024, 23:28 pm

Diwani wa kata ya Ndumbwe ambae pia mwenyekiti wa CUF wilaya ya Mtwara Abdull Mahupa akitoa taarifa kwa mwongoza kikao juu ya kususia kwa kikao hicho (Picha na Musa Mtepa)

Inaelezwa kuwa sababu kubwa ya kususia kikao hicho ni kwa kile walichokiita kutotendewa haki kwa wagombea wao kwa kuwaondoa katika orodha ya wagombea wa nafasi za uongozi katika uchaguzi wa serikali za mitaa kwa kosa la kujaza vibaya fomu.

Na Musa Mtepa

Leo, Novemba 8, 2024, madiwani 10 wa vyama vya upinzani wa halmashauri ya Mtwara  wamesusia kikao cha Baraza la Madiwani.

Hatua hiyo inatokana na kile wanachoeleza kuwa kutokubaliana na maamuzi ya msimamizi wa uchaguzi wa halmashauri hiyo, ambaye amewaengua baadhi ya wagombea wa nafasi ya uenyekiti kwa madai ya kujaza vibaya fomu za uteuzi wa wagombea.

Diwani wa kata ya Ndumbwe ambae pia ni Mwenyekiti wa CUF wilaya ya Mtwara, Abduly Bakari Mahupa, amesema wamechukua hatua ya kususia kikao hicho kutokana na matukio ya kiuchaguzi ambayo hayakuridhisha.

Ameeleza kwamba wagombea wao wameondolewa kwenye uchaguzi kwa sababu ya kushindwa kutimiza vigezo, ikiwemo kujaza vibaya fomu.

Sauti ya Abdully Bakari Mahupa Diwani kata ya Ndumbwe na Mwenyekiti wa CUF wilaya

Patrick Simwinga, Diwani wa kata ya Nanguruwe kutoka CHADEMA, amekosoa hatua hiyo, akisema ni vigumu kukubali kuwa sehemu ya kikao hicho ili hali watu wao waliotumia haki yao ya kidemokrasia na nguvu zao ya kuwa sehemu ya uchangiaji wa michango ya kimaendeleo kwenye vijiji vyao ya kuwa wenyeviti na wajumbe wanaenguliwa.

Sauti ya Patrick Simwinga Diwani wa kata ya Nanguruwe

Katibu wa ACT-Wazalendo  Mtwara Vijijini, Hamisi Likwenda, Likwenda amesema anaunga mkono kitendo cha kususia kikao kilichofanywa na Madiwani .

Sauti ya Hamisi Likwenda katibu wa ACT-WAZALENDO Mtwara vijijini

Kwa upande mwingine, Makamu Mwenyekiti wa halmashauri ya Mtwara Vijijini, Abdala Saidi Makame, amekosoa kitendo cha madiwani hao kutoshiriki kikao, akisema kuwa ni utovu wa nidhamu huku akiwataka warudi kwenye viti vyao.

Sauti ya Abdala Saidi Makame makamu mwenyekiti wa halmashauri.

Msimamizi Mkuu wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa halmashauri ya  Mtwara, Abeid Abeid Kafunda, ameeleza kuwa hajapokea malalamiko rasmi ya kimaandishi na kuwasihi viongozi wa vyama vya upinzani, wanapokuwa na malalamiko, kuwasiliana na maafisa wa uchaguzi ili kuhakikisha mchakato unafanyika kwa amani na haki.

Sauti ya Abeid Abeid Kafunda msimamizi mkuu wa uchaguzi wa serikali za mitaa Mtwara Dc.