Wananchi walia na huduma za uzazi Mtwara DC
7 August 2024, 11:21 am
Kutokana na wahudumu kuwa wachache katika zahanati ya Kijiji cha Kawawa wakati mwingine Wagonjwa hususani akina mama wajawazito wanalazimika Kwenda mjini ua Nanguruwe kupata huduma ya afya kwa kuamini kuwa wanaweza kupata huduma kwa uharaka kutokana na kuwepo kwa Wahudumu wengi.
Na Musa Mtepa
Wananchi wa Kijiji cha Kawawa kata ya Mkunwa Halmashauri ya Mtwara Vijijini wameiomba Serikali kuwaongezea wahudumu wa afya Pamoja na kuwajengea jengo la kujifungulia katika Zahanati ya Kijiji hicho.
Wakizungumza na jamii fm redio wananchi hao wamesema kuwa Wahudumu waliopo wanafanya kazi mzuri lakini wakati mwingine wanazidiwa na wagonjwa hivyo serikali iangalie kwa jicho la tatu changamoto hiyo ili kuwarahisishia wagonjwa kupata huduma iliyo bora Pamoja na kupata muda wa kupumzika wahudumu wawili waliopo katika Zahanati hiyo inayohudumia zaidi ya vijiji vitano.
Bibi Sofia Chikaya na Sofia Palangadau wakazi wa Kijiji hicho wamesema kutokana na uwepo wa wahudumu wachache katika Zahanati hiyo wanaiomba serikali kuwaongezea wahudumu hususani wa kike Pamoja na kuwajengea jengo maalumu la huduma ya mama na uzazi ili kuepuka kadhia wanayokutana nayo hivi sasa.
Naye Bi Lukia Chitenda Mkazi wa Kijiji cha Kawawa amesema kuwa huduma zinazotolewa ni mzuri ila changamoto ipo kwa upande wa huduma za kujifungulia kutokana na vifaa vilivyopo kutokukidhi mahitaji ya wajawazito wanaofika katika Zahanati hiyo.
Akizungumza kwa njia ya Simu Mwenyekiti wa Kijiji cha Kawawa Himidi Bakari Namakanya amethibitisha uwepo wa changamoto hizo huku akisema kuwa wamekuwa wakilizungumzia kwenye vikao vya Kijiji na kata katika kuona namna gani wanaweza kutatua changamoto hizo.