NEMC Kanda ya Kusini yashiriki zoezi la upandaji wa mikoko Namela
5 June 2024, 16:47 pm
Kati ya miti ambayo inafyonza hewa chafu kwa uwingi na kwa haraka ni mikoko hivyo kitendo cha kupanda katika eneo la kigongo ni katika kuendeleza harakati za kupunguza hewa chafu na ni fursa kwa maeneo mengine ya pwani ya kusini kuwa na utaratibu wa upandaji wa miti hii
Na Musa Mtepa
Meneja wa Baraza la Taifa la Uhifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Kanda ya Kusini Mhandisi Boniphace Guni Juni 4, 2024 ameshiriki zoezi la upandaji wa mikoko eneo la Kigongo katika kijiji cha Namela kata ya Msangamkuu wilaya na mkoani Mtwara.
Zoezi hilo lililohusisha vijana wa Madrasat Sabilia tawi la Msangamkuu,umoja wa usimamizi wa rasilimali za bahari (BMU) Namela Pamoja na viongozi wa serikali ya Kijiji
Akizungumza baada ya zoezi la upandaji kukamilika meneja wa NEMC kanda ya kusini Mhandisi Boniphace Guni amefurahishwa na jitihada zilizofanywa na BMU Kijiji cha Namela kwa kitendo cha kutunza mazingira eneo la kigongo katika hali ya asili huku akiiomba jamii kushirikisha vijana ili baadae waweze kuwa mabalozi wazuri katika utunzaji wa mazingira.
Aidha Mhandisi Guni amememuomba mtendaji wa Kijiji cha Namela Pamoja na viongozi wa BMU kuhakikisha mikoko iliyopandwa katika eneo hilo inalindwa na kutunza ili jitihada zilizofanyika zisipotee bure.
Kwa upande wake Kulwa Issa Saidi katibu wa jumuia ya umoja wa usimamizi wa rasilimali za Bahari (BMU) kata ya Msangamkuu amesema katika kuahakikisha eneo la pwani linakuwa safi wamekuwa wakifanya usafi katika eneo la fukwe,kulima kilimo cha Mwani Pamoja na kupanda mikoko ikiwa njia mojawapo ya kutunza mazingira.
Naye Ostadhi Mubaraka Juma kutoka Madrasat Sabilia amesema kuwa hata kwa viongozi watukufa wa dini wameelezea umuhimu wa kutunza mazingira hivyo wao kama viongozi wa kiimani watahakikisha wanashirikiana na vijana katika kulinda na kutunza mazingira kama maandiko yanavyoelezea.